1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na Armenia zarejesha uhusiano baina yao

Miraji Othman11 Oktoba 2009

Uhasama KWISHA baina ya Uturuki na Armenia

https://p.dw.com/p/K44a
Waziri wa mambo ya kigeni wa Armenia, Eduard Nalbandian(kushoto), akipeana mkono na waziri mwenzake wa Uturuki, Ahmed Davutoglu, baada ya wote wawili kutia saini mkataba wa nchi zao kuwa na uhusiano wa kawaida huko Zürich, Uswissi.Picha: AP

Baada ya kupita miaka 16 ya kunyamaziana, Uturuki na Armenia sasa zinataka tena kurejesha uhusiano wao uwe katika hali ya kawaida. Baada ya kupita mwaka mzima wa kuendeshwa diplomasia ya kisirisiri, itifaki juu ya jambo hilo ilitiwa saini jumamosi iliopita katika Chuo Kikuu cha Zürich, nchini Uswissi, na mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi hizo mbili. Sherehe hiyo ya kutiwa saini, ambayo pia ilihudhuriwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, na wenzake wa kutokea Russia na Ufaransa, na pia mwakilishi wa masuala ya siasa za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, ilikuwa karibu ivunjike kutokana na malalamiko ya upande wa Armenia. Nusura ilipatikana tu kutokana na pande zote mbili kuachana na mpango wa kutaka kutoa hotuba zao za mwisho kwenye sherehe hiyo, na pia kutokana na kujiingiza binafsi Hillary Clinton. Katika itifika zilizotiwa saini, pande zote mbili zilitangaza nia zao za kuanzisha uhusiano wa kibalozi na kuifungua mikapa baina ya nchi zao mbili mnamo miezi miwili ijayo. Licha ya hayo, tume ya kihistoria itatayarisha hatua za kuchukuliwa ili lidurusiwe upya suala la mauaji waliofanyiwa Wa-Armenia wakati wa wa utawala wa Waturuki baina ya mwaka 1915 hadi 1917.

Mkataba huo unabidi upewe idhini ya mwisho na mabunge ya nchi zote mbili.

Kuacha mawaziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki na Armenia, Ahmet Davutoglu na Eduard Nalbandian, kutoa hotuba walizopanga baada ya kutiwa saini itifaki za mkataba wa kurejesha kuwa wa kawaida uhusiano baina ya nchi zao mbili, ilikuwa ni ishara ndogo. Lakini kazi ya mbele ni kubwa. Kabla ya mkataba huo wa Zürich kukubaliwa na kupewa idhini ya mwisho na mabunge ya huko Ankara na Eriwan, mkataba huo utakabiliana na upinzani mkubwa, na kwa sehemu utabidi uyakiuke malalamiko makubwa ya wazalendo wa nchi zote mbili. Hata siku ya kabla kutiwa saini mkataba huo, Wa-Armenia 10,000 walikwenda mabarabarani katika mji mkuu wa nchi yao, Eriwan. Hata hivyo, juhudi za kutaka kuufungua mpaka uliofungwa na Uturuki hapo mwaka 1993- jambo lenye umuhimu wa kiuchumi kwa Armenia- bado haziko katika uhakika. Pia sio hakika kama na lini uhusiano wa kibalozi baina ya nchi hizo mbili, ambao ulivunjika kutokana na mzozo wa eneo la Mlima wa Karabach lililoko Azerbaijan, utaweza kurejeshwa.

Hata hivyo, kwa vyovyote, Uswissi, kama mpatanishi, pia Marekani, Russia na Ufaransa, kama wasaidizi katika mwenendo huu mgumu wa amani, zimefikia hatua muhimu. Suali ni : mambo yatakwenda vipi kutokea hapa? Itategemea kila neno litakalotamkwa, na ndio maana mawaziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki na Armenia wakaamuwa kwamba saini zao zisiambatanishwe na hotuba za hoja wanazozishikilia.Yote ni kwamba nia ya hatua hiyo ifuatwe na amani. Waziri wa mambo ya kigeni wa Armenia, ambaye hataelezea wazi wazi malalamiko ya nchi yake kuhusu mauaji yaliofanywa na Uturuki, au waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki, ambaye hatalaani hatua ya Armernia ya kuikalia ardhi ya Azerbaijan, wote wawili basi watakuwa katika hatari ya kupoteza kuaminika katika nchi zao wenyewe.

Umoja wa Ulaya, ukiwakilishwa na mwanadiplomasia wake mkuu, Javier Solana, na kama kuutambuwa mkataba huu, umeziahidi Uturuki na Armenia kuwa na uhusiano ulio bora zaidi na nchi hizo mbili. Ni bahashishi ya namna hiyo, ndio maana wazalendo wa nchi zote mbili wanauita mkataba huu kuwa ni uhaini. Wenye siasa kali katika Uturuki wanakumbusha juu ya wanadiplomasia 37 wa Kituruki waliouliwa duniani kote kutokana na mashambulio ya kikundi cha kigaidi cha Wa-Armenia, ASALA, na wameonya juu ya kuwafanyia uhaini ndugu zao wa Azerbaijan. Na kwa wazalendo wa Ki-Armenia, pia walioko ng'ambo, kuwa na uhusiano wowote wa kawaida na Uturuki, bila ya Uturuki kuyatambua mauaji ya halaiki ilioyafanya dhidi ya Wa-Armenia mwaka 1915 hadi 1917 ni jambo lisilokubalika.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi zote mbili wamebishana vikali kuja na kila neno lililomo katika mkataba huo, na kazi ngumu itakuwa kuyashawishi mabunge na wananchi katika nchi zote mbili. Lakini isikubaliwe kuupa mgongo mwenendo huu wa amani. Kwa hivyo, unahitajika msaada zaidi , na, ikiwa lazima , basi mbinyo unaofaa kutoka upande wa Umoja wa Ulaya, Marekani na Ufaransa ambazo zina Wa-Armenia wengi walio ng'mabo, na pia Russia. Zama za Vita Baridi katika Ulaya zimekwisha, na hali hiyo pia iwe ya zamani katika sehemu za pembezoni mwa Bara la Ulaya.

Mwandishi : Güngör, Baha/ Othman, Miraji / ZR

Mhariri: Martin, Prema