1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki, Uganda kuongeza ushirikiano

Admin.WagnerD2 Juni 2016

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesaini makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara, utalii, ulinzi, elimu na uhamiaji na rais wa Uganda Yoweri Museveni kufuatia ziara ya siku mbili nchini humo.

https://p.dw.com/p/1IymG
Afrka Uganda Erdogan
Picha: Getty Images/AFP/P. Busomoke

Rais Erdogan ambaye yuko katika mkondo wake wa tatu wa ziara barani Afrika mwaka huu, ametoa shukurani kwa Uganda kwa usaidizi wake wakati janga la ebola lilipoikumba Afrika magharibi kwani wataalamu wa afya wa nchi hiyo walifanya kazi kubwa kuchangia katika kulidhibiti.Uturuki ilikuwa imeahidi kutoa mchango wa dola milioni tano kwa shughuli hiyo.

Aidha ameitaja Uganda kuwa mbia muhimu katika juhudi za kuleta amani nchini Somalia akisema kwamba nchi yake itaendelea kujihusisha na juhudi hizo kwani raia wa Somalia wangali wanahitaji msaada wa kimataifa.

Rais Erdogan ambaye aliwasili Jumanne jioni ameukosoa Umoja wa Ulaya kwa kupunguza ufadhili wake kwa shughuli za kuleta amani nchini Somalia chini ya mpango wa AMISOM ambamo Uganda ni mshiriki mkuu kwa kuchangia zaidi ya wanajeshi 5,000.

Rais Erdogan akikagua gwaride la heshima baada ya kuwasili katika ikulu ya rais mjini Entebbe.
Rais Erdogan akikagua gwaride la heshima baada ya kuwasili katika ikulu ya rais mjini Entebbe.Picha: Getty Images/AFP/P. Busomoke

Uganda yatafakari uwepo wake Somalia

Umoja wa Ulaya umekuwa ukitoa mchango wa takriban dola milioni 200 kila mwaka kwa shughuli za kukabiliana na wapiganaji wa Al shabaab wanaodaiwa kuungwa mkono na kundi la kigaid la Al Qaeda. Hivi karibuni umoja huo ulitangaza kupunguza kiasi hicho kwa aslimia 20 na athari za hatua hii zimeanza kuonekana kwani wanajeshi wa Uganda hawajapokea malipo kwa zaidi ya miezi sita.

Hii imepelekea Uganda kuanza kuchughuza upya uhusika wake katika mpango wa AMISOM jambo ambalo limefasiliwa na baadhi ya wadadisi kuwa maandalizi ya nchi hiyo kuondoa majeshi yake Somalia.

Mara kadhaa rais huyo wa Uturuki amenukuliwa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa akiushtumu Umoja wa Ulaya kuhusu masuala mbalimbali hasa baada ya juhudi za nchi hiyo kujiunga na umoja huo kukwama kwani viongozi wa umoja huo wangali wana mtazamo kwamba utawala wake unakiuka haki za binadamu na hawako tayari kushirikiana na uongozi ambo baadhi wameutaja kuwa wa udikteta.

Hivi karibuni Uturuki imekuwa mbioni katika kufungua balozi Afrika na kwa sasa ina vituo 39 vya ubalozi barani humo. Rais Erdogan amelezea hilo kuwa mkakati wao Uturuki kushirikiana zaidi na mataifa ya bara hilo ili yaimairishe maendeleo yao ya kiuchumi, kuwepo kwa amani na pia usalama.

Rais Erdogan akimkabidhi rais museveni kitabu chake dira ya amani kwa Dunia.
Rais Erdogan akimkabidhi rais museveni kitabu chake dira ya amani kwa Dunia.Picha: picture-alliance/AA/K. Ozer

Makubaliano ya ushirikiano

Akikamilisha ziara yake Alhamisi asubuhi, rais Erdogan alisaini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara,utalii, ulinzi,elimu na uhamiaji na mwenyeji wake rais Museveni. Kufuatia makubaliano hayo, Uturuki itawekeza dola milioni 600 katika ujenzi wa mtaa wa viwanda vya kusindika bidhaa za vyakula, zile za kutengeneza bidhaa za matumizi ya umeme nyumbani kama vile televisheni na pia katika utengenezaji wa nishati.

Biashara kati ya Uturuki na mataifa ya bara Afrika kusini mwa jangwa la sahara imestawi mara kumi tangu mwaka 2000. Lakini kwa mtazamo wa wadadisi wa masual ya kisiasa, Uturuki nayo inalenga kujiweka katika nafasi ya kuwa na ushawishi mkubwa barani afrika kisiasa na kiuchumi baada ya kucheleweshwa kujiunga na umoja wa ulaya.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.

Mhariri: Iddi Ssessanga