1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaendeleza mashambulizi dhidi ya Wakurdi Syria

Grace Kabogo
11 Oktoba 2019

Ndege za kivita za Uturuki na makombora zimeyashambulia maeneo ya wanamgambo wa Kikurdi kaskazini mashariki mwa Syria.

https://p.dw.com/p/3R7gE
Syrien Konflikt Grenze Türkei | Explosion in Tel Abyad
Picha: Reuters TV

Zimetimia siku tatu tangu Uturuki ilipoanzisha operesheni hiyo ya kijeshi ambayo hadi sasa imesababisha mamia ya watu kuuawa na kuwalazimisha wengine maelfu kuyakimbiaa makaazi yao. Mapema leo asubuhi, Uturuki imelishambulia eneo la Ras al Ain, moja ya miji miwili iliyoko mpakani ambayo imekuwa ikilengwa katika operesheni hiyo ya kijeshi.

Msafara wa magari 20 ya kivita yakiwa na waasi wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki yaliingia Syria yakitokea Ceylanpinar, huku baadhi yao wakionyesha ishara ya ushindi na kusema Mungu ni mkuu. Waasi hao walionekana wakipeperusha bendera ya Syria wakati wakielekea Ras al Ain.

Mashambulizi yaanza tena

Mmoja wa watu aliyeshuhudia amesema Uturuki ilianzisha tena mashambulizi karibu na mji wa Tel Abyad. Msemaji wa vikosi vya Kikurdi vinavyopigania demokrasia nchini Syria, SDF, Marvan Qamishlo amesema katika muda wa siku tatu mji wa Tel Abyad unashuhudia mashambulizi makali zaidi. Qamishlo amesema eneo lote la mpakani lilikuwa katika mashambulizi makali.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imesema watu 64,000 wa Syria wameyakimbia makaazi yao tangu kuanza kwa mashambulizi hayo. Miji ya Ras al Ain na Darbasiya iliyoko umbali wa kilomita 60 kuelekea mashariki, imebakia bila watu.

Syrien Tel Abyad | Konflikt Grenze Türkei | Syrische Kämpfer, unterstützt durch Türkei
Vikosi vinavyoungwa mkono na Uturuki vikiingia Tel Abyad Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Wizara ya Ulinzi ya Uturuki, imesema wakati wa operesheni ya kijeshi pamoja na waasi washirika wao, jumla ya wapiganaji 49 wa Kikurdi wameuawa. Kwa mujibu wa wizara hiyo, hadi sasa idadi jumla ya wanamgambo waliouawa ni 277. Wizara hiyo imesema askari mmoja wa Uturuki ameuawa katika mashambulizi hayo yanayovilenga vikosi vya SDF ambayo yanaongozwa na kundi la wanamgambo wa Kikurdi, YPG.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Maqdad amesema hakuna mazungumzo yoyote kati ya nchi yake na vikosi vya Kikurdi vinavyoungwa mkono na Marekani, kwa sababu vilikataa kushiriki katika meza ya mazungumzo.

''Hivi vikosi mnavyovizungumzia vilikataa njia zote za mazungumzo na badala yake vikafungua mlango kwa Uturuki kufanya kile inachokifanya. Milango ya serikali ya Syria iko wazi kwa wananchi wake wote, lakini hakuna njia ya kufanya mazungumzo na waasi, sio kwa mantiki ya kujitenga au kwa dhana kwamba wao wana nguvu thabiti,'' alifafanua Maqdad.

Vijiji kadhaa vyadhibitiwa

Kundi linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria limesema wapiganaji wapatao 29 wa SDF na wapiganaji 17 wa YPG wameuawa. Kundi hilo limesema vikosi vya Syria vimevidhibiti vijiji viwili karibu na Ras al Ain na vijiji vitano karibu na Tel Abyad.

Hata hivyo, Qamishlo amesema miji hiyo ilizungukwa baada ya wapiganaji kuvidhibiti vijiji karibu na wao. SDF imesema mashambulizi hayo yamewaua raia tisa. Maafisa wa Uturuki wamesema katika shambulizi la kulipiza kisasi vikosi vya Kikurdi vimewaua watu sita, akiwemo mtoto wa miezi tisa.

Brüssel Jens Stoltenberg, NATO-Generalsekretär
Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/D. Aydemir

Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg ameelezea wasiwasi wake kuhusu mashambulizi hayo dhidi ya vikosi vya Kikurdi.

Akizungumza na waandishi habari mjini Istanbul pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, Stoltenberg ametoa wito kwa pande zote kujizuia. Hata hivyo, Uturuki imesema inategemea kupata mshikamano kutoka NATO badala ya vitisho.

Rais wa Urusi Vladmir Putin ametahadharisha kuwa wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS wanaweza kutoroka jela katika eneo la kaskazini mashariki mwa Syria kutokana na operesheni hiyo inayoendelea.

Wakati huo huo, Ufaransa imesema Umoja wa Ulaya utajadili vikwazo vya Uturuki wiki ijayo kutokana na hatua yake ya kuanzisha operesheni nchini Syria.

(AFP, DPA, AP, Reuters)