1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yatuma majeshi Irak

Kalyango Siraj22 Februari 2008

Wapiganaji wanadai wanajeshi kadhaa wameuliwa na wengine kujeruhiwa

https://p.dw.com/p/DBv6
Helikopta ya jeshi la Uturuki ikiruka katika eneo la milima ya Yuksekova karibu na mpaka wa IrakPicha: picture-alliance/ dpa

Majeshi ya Uturuki yameingia Iraq kusaka wapiganaji wa kikurdi wa chama cha PKK. Hatua hiyo imepokelewa kwa njia tofauti.Huku Marekani ikisema ilijua kuhusu hatua hiyo kabla ya kutekelezwa Umoja wa Ulaya umeionya Uturuki kuwa na uangalifu wakati inapotekeleza malengo yake.

Uturuki imetuma wanajeshi elf 10 wa nchi kavu nchini Iraq kupambana dhidi ya wapiganaji wa kikurdi wanaotumia Iraq kama maficho kuishambaulia Uturuki.

Inasemekana hii ndio mara ya kwanza kwa nchi hiyo kutuma wananjeshi wa nchi kavu kiasi hicho nchini Iraq kwa lengo la kukabiliana na wapiganaji hao.

Mashambulio mengi ya Uturiki dhidi ya wapiganaji hao yamekuwa kutumia mizinga, ndege za kijeshi na wakati ikilazimika kutumia askari wa nchi kavu wachache.

Taarifa ya idadi ya wanajeshi walioingia Iraq imetolewa na kituo cha televisheni cha kibnafsi nchini Uturuki cha NTV.

Baadae makao makuu ya jeshi, kupitia taarifa ambayo iliwekwa katika tovuti ya serikali, yalihakikisha habari za majeshi yake kuingia Iraq, lakini bila kutoa idadi ya wanajeshi waliohusika.

Taarifa ya jeshi ilisema kuwa operesheni hiyo itakuwa si kali na majeshi yataondoka haraka inavyowezekana.

Kituo cha televisheni cha NTV kilisema kuwa wanajeshi hao walikuwa umbali wa kilomita 10 ndani mwa Iraq kutoka mpakani wakati wa saa za mchana.

Hatua hii ikiwa inaungwa mkono na raia wa Uturuki kamishna wa masuala ya nje wa Umoja wa Ulaya-Javier Solana-amesema kuwa hatua ya jeshi la Uturuki ya kuwasakama wapiganaji wa PKK-kaskazini mwa Iraq sio njia pekee nzuri ya kukabiliana na mashambulizi ya wapiganaji hao.Aidha amesema kuwa mipaka ya Iraq ni lazima iheshimiwe.

Jeshi la Uturuki linasema licha ya kufanya operesheni hiyo lakini baado linatilia maanani uhuru wa mipaka ya Iraq.

Nao kwa upande wao, wapiganaji wa kituruki wa PKK, wanadai kuwa tangu majeshi ya Uturuki yanze hujuma dhidi yao hiyo jana,wameweza kuwauwa wanajeshi wawili na kuwajeruhi wengine wanane.Hata hivyo maafisa wa Uturuki hawakuhakikisha mapema madai hayo.

Yeye msemaji wa kundi la Kurdistan Workers Party-maarufu kama PKK-Ahmad Danas amesema kuwa wapiganaji wake walikuwa wamejiandaa kwa hujuma za majeshi ya ardhini ya Uturuki,baada ya mashambulizi ya mizinga na ndege ya hapo hapo jana.

Msemaji wa jeshi la Marekani amesema kuwa anaamini kuwa hatua hii ya jeshi la Uturuki haitachukua mda mrefu.

Aidha kuna habari kuwa Marekani ilikuwa na habari za hatua hii hata kabla ya kutokea.

Rais wa Uturuki,Abdullah Gul, kupitia taarifa,anasema alimpigia simu mwenzake wa Iraq-Jalal Talaban na kumuarifu kuhusu mashambulio ya mizinga na ndege za kijeshi dhidi ya maeneo yanayofikiriwa kuwa maficho ya wapiganaji wa PKK nchini Iraq.Pia inasemekana rais wa Uturuki alimualika mwenzake wa Iraq kuitembelea Uturuki.

Hata hivyo hakumfahamisha kuhusu hatua ya majeshi yake ya ardhini kuingia kaskazini mwa Iraq.