1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uvumi waenea kuhusu ziara ya Kim Jong-un Beijing

Iddi Ssessanga
27 Machi 2018

Uvumi kuhusu ziara ya kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un mjini Beijing umehanikiza katika wakati ambapo kukiwa na gumzo kuhusu maandalizi ya mkutano wa kilele kati ya kiongozi huyo wa Korea Kaskazini na rais Trump.

https://p.dw.com/p/2v3OS
Nordkorea Führer Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/AP Photo/Wong Maye-E

Mji Mkuu wa China Beijing, ulikuwa chini ya usalama mkali Jumanne, huku kukiwa na uvumi kwamba kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un alikuwa anafanya ziara ya kustukiza, kufuatia ripoti za kuwasili kutoka Pyongyang, kwa treni maalumu iliyopokelewa kwa gwaride la heshima.

Ikiwa itathibitika, hii itakuwa ziara ya kwanza ya nje ya Kim tangu alipoingia madarakani mwaka 2011, na inaashiria mabadiliko ya kushangaza katika zoezi la kidiplomasia ambalo limefungua mlango wa mikutano tofauti ya kilele kati ya Kim na marais wa Korea Kusini na Marekani.

Baadhi ya wachambuzi wanasema China -- mshirika pekee mkubwa wa Korea Kaskazini -- ilikuwa imewekwa kando katika mazugumzo ya awali ya Pyongyang na Korea Kusini na Marekani, lakini ziara ya Kim itairudisha Beijing katika mlinganyo wa kidiplomasia.

Sonderzug von Kim Jong Un
Treni maalumu inayotumiwa na familia ya kina Kim nchini Korea Kaskazini.Picha: picture alliance/dpa/kyodo

Bill Bishop, mchapishaji wa jarida la habari la Cinocism China, amesema rais Xi Jinping huenda alitaka kukutana na Kim kabla ya mkutano wa kilele na Rais Donald Trump, ambao unatazamiwa kufanyika mwezi Mei.

Bishop amlimabia shirika la habari la AFP kwamba Wachina wanahofia kuachwa nje wakati Korea Kaskazini ikitafuta kufikia makubaliano ya moja kwa moja na Marekani ambayo hayaakisi maslahi ya China.

Usiri mkubwa

Uwezekano wa ziara hiyo uliripotiwa kwa mara ya kwanza na shirika la habari la Japan la Kyoto, likinukuu vyanzo ambavyo halikuvitaja vikisema kwamba afisa wa ngazi ya juu wa Korea Kaskazini alikuwa amewasili katika mji mkuu wa China usiku wa Jumatatu.

Kituo cha Televisheni cha Nippon cha nchini Japan kilitangaza picha za video zikionesha treni inayofanana na ile iliyokuwa ikitumiwa na yake Kim, marehemu Kim Jong Il -- ikiwasili katika kituo cha treni cha Beijing na kupokelewa kwa heshima za kijeshi na msafara wa magari ya rangi nyeusi.

Katika nyumba ya wageni ya Diaoyutai, ambako Kim Jong Il alikuwa akiishi wakati wa ziara zake mjini Beijing, kulikushuhudiwa uwepo mkubwa wa polisi isivyo kawaida, ambapo maafisa walikuwa wamewekwa kila baada ya mita 50 hadi 100 mbele ya jengo la kuvutia.

China Spekulationen über Geheimbesuch von Kim Jong Un in Peking
Polisi wakizuwia mtaa mjini Beijing, unaolekea katika nyumba ya wageni ya serikali ya Diaoyutai, ambako usalama ulikuwa umeimarishwa.Picha: picture-alliance/dpa/AP/M. Schiefelbein

Hakukuwa na utajo wa ziara yoyote katika vyombo vya habari vya ama China au Korea Kaskazini, na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Hua chunying, alipoulizwa iwapo Kim au afisa mwingine wa Korea Kaskazini alikuwa anaizuru Beijing, alisema hana taarifa kuhusu suala hilo.

Ziara za huko zilizofanywa na Kim Jong Il nchini China zilikuwa pia zikigubikwa na usiri, ambapo Beijing ilikuwa ikithibitisha uwepo wake baada ya kuvuka mpaka na kurudi Korea Kaskazini kwa usafiri wa treni.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape, afptv,dpae.

Mhariri: Mohammed Khelef