1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado mshukiwa mmoja wa Ugaidi anasakwa Ubelgiji

Mjahida30 Machi 2016

Uwongozi wa uwanja wa ndege wa Brussels umesema hautaufungua uwanja huo licha ya majaribio ya kufungua tena huduma katika uwanja huo kufanyika, Baada mashambulio ya kigaidi yaliyosababisha mauaji ya watu 32.

https://p.dw.com/p/1IM4S
Belgien Brüssel nach Terroranschlägen
Afisa wa polisi akielekeza magari karibuna uwanja wa ndege wa ZaventemPicha: DW/M. Hallam

Uwanja wa ndege wa Zaventem ulifungwa tangu kutokea kwa milipuko miwili katika uwanja huo tarehe 22 mwezi Machi katika mashambulio yanayodaiwa kupangwa na kundi la dola la kiislamu IS yaliyokitikisa pia kituo cha teni cha Maalbeek katikati mwa mji wa Brussels.

Watu 32 waliuwawa katika shambulio hilo linalosemekana kuwa baya zaidi huku serikali ikisema imeshusha idadi ya vifo kutoka 35 hadi 32 kufuatia taarifa za kukanganya kuhusu watu wawili waliyofariki kwenye eneo la tukio na hospitalini.

"Baada ya kutathmini taarifa na kuzithibitisha kwa kina idadi ya waliyofariki imeshuka hadi 32, bado watu 94 wako hospitalinil," alisema Waziri wa Afya Maggie de Block aliyetoa maelezo hayo kupitia mtandao wa kijamii wa twitter.

Brüssel - Gedenken an die Opfer der Anschläge.
Raia wa Ubelgiji, waweka maua katika eneo la shambulio la kigaidi.Picha: DW/B. Riegert

Hapo jana wafanyakazi kadhaa wa uwanja huo wa ndege walirejea kazini kufanya majaribio ya kuufungua tena hii leo lakini matumaini yao yakazimwa, baada ya msemaji wa uwanja huo Anke Fransen kusema bado utawala unatathmini jaribio lililofanyika akiongeza kuwa wanatumai kufikia uamuzi baadaye leo.

Hata hivyo mkurungenzi mkuu wa uwanja wa ndege wa Zaventem Arnaud Feist ameonya huenda ikachukua miezi kadhaa kwa operesheni huko kurejea kama kawaida. Kwa upande wake shirika la ndege la Brussels limesema linapitia mgogoro mkubwa katika historia yake kwa sababu ya kufungwa uwanja huo kwa kupoteza euro milioni tano kwa siku.

Bado Brussels iko mbioni kumkamata mshukiwa wa Ugaidi

Wakati Brussels ikijaribu kujikwamua tena baada ya shambulio hilo la kigaidi serikali ya Ubelgiji imeendelea kukosolewa namna inavyoshughulikia suala hili, baada ya mtuhumiwa aliyeshitakiwa kuhusiana na mashambulio hayo Faycal Cheffou kuachiwa huru siku ya Jumatatu kwa kukosekana ushahidi katika kesi yake.

Lakini kwa sasa juhudi za kumkamata mshukiwa aliyevalia kovia aliyeonekana kupitia kamera za CCTV karibu na watu wawili waliohusika katika mashambulizi hayo katika uwanja wa ndege zinaendelea.

Schaubild Terrornetzwerk Belgien anderer Ausschnitt
Washukiwa wa Ugaidi BrusselsPicha: DW/B.Riegert

Huku hayo yakiarifiwa Uholanzi imesema maafisa wake wa ujasusi walitoa taarifa kwa Ubelgiji juu ya washambuliaji wa Brussels siku sita kabla ya tukio kutokea.

Kulingana na Waziri wa sheria wa Uholanzi Ard van der Steur ripoti hiyo ya maafisa wake wa ujasusi ilihusu rekodi ya uhalifu wa kigaidi ya Ibrahim El Bakraoui na kakaake.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri:Iddi Ssessanga