1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uzalishaji kwa wingi kupitia upasuaji watajwa kuwa janga

12 Oktoba 2018

Mamilioni ya wanawake wanajifungua kwa njia ya upasuaji badala ya kawaida, bila ya kuwepo kwa hatari yoyote inayowalazimu kufanya hivyo, kulingana na utafiti uliofanywa na madaktari.

https://p.dw.com/p/36QsO
USA Chirurgie Zimmer
Picha: picture alliance/dpa/epa/Lightchaser Photography/Brigham and Womens Hospital

Viwango vya dunia vya wanawake kujifungua kupitia upasuaji viliongeza mara mbili kati ya mwaka 2000 na 2015, huku mara nyingi upasuaji huo ukifanywa bila ya kuwa na umuhimu au manufaa yoyote ya uzazi. Upasuaji unaweza kuokoa maisha yawanawake na watoto wakati kuna matatizo ya uzazikama vile dhiki kwa kijusi au kijusi kuwa katika nafasi isiyo ya kawaida.

Hata hivyo utafiti huo wa madaktari uliochapishwa katika jarida la masuala ya afya, The Lancet, limesema iwapo upasuaji utakuwa chaguo la kila mara kwa wanawake wanaotaka kujifungua, huenda ikasababisha athari za muda mrefu na gharama za juu za huduma za afya. Wataalamu wanatathmini kuwa kati ya asilimia 10 na 15 ya wanawake wanajifungua kupitia upasuaji kutokana na matatizo ya kiafya.

USA Chirurgie Zimmer
Picha: picture alliance/dpa/epa/Lightchaser Photography/Brigham and Womens Hospital

Kwa kuzingatia data za Shirika la Afya Duniani na Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto UNICEF kutoka mataifa 169,utafiti huo ulibaini tofauti kubwa kati ya maeneo ya Kijiografia, huku asilimia sitini ya mataifa hayo yakiitumia vibaya upasuaji na asilimia 25 wakiitumia njia hiyo ya upasuaji kwa kiwango kidogo.

Katika mataifa kumi na tano, zaidi ya asilimi 40 ya waliozalishwa walipitia upasuaji, huku Jamhuri ya Dominika ikiongoza kwa asilimia 58.1 ya watoto waliozaliwa kupitia njia ya upasuaji. Katika mataifa ya Brazil, Misri na Uturuki zaidi ya nusu ya watoto wanazaliwa kupitia upasuaji, na katika maeneo ya Magharibi na Afrika ya Kati upasuaji ulitumika tu kwa asilimi 4.1.

Utafiti huo wa madaktari aidha umeonesha kuwa upasuaji unaweza kuchangia athari kubwa katika miaka ijayo kukiwemo vizazi vya baadaye, kama vile kovu la tumbo, kuharibika kwa uterasi, kondo lisilo la kawaida, ujauzito ulio nje ya uterasi, watoto kuzaliwa wakiwa wamekufa au kabla ya siku zao. Vilevile imethibitishwa kuwa upasuaji unaweza kuwa na kuathari homoni, mwili na kinga ya mwili ya mtoto.

China Tattoos Kaiserschnitt
Picha: Reuters/A. Song

Utafiti huo aidha umesema kuwa wanawake wanahamasishwa kujifungua kupitia upasuaji kwa sababu ya matatizo waliyoyapata walipojifungua kwa njia ya kawaida, woga, maumivu au kupungua kwa hamu ya kushiriki mapenzi. Katika baadhi ya nchini upasuaji umekuwa mtindo na kuchukuliwa kuwa wa kisasa au salama.

Watafiti wanasema kuna haja ya hatua ya haraka kuchukuliwa katika nyanja ya matibabu kupunguza idadi ya wanawake wanaojifungua kupitia upasuaji. Kadhalika wamependekeza wanawake wapewe taarifa zaidi na ushauri kuhusu upasuaji, pamoja na kuongezwa kwa huduma ya uzawa, na kuhakikisha madaktari wanatoa sababu ya kutosha kabla ya kuamua kumzalisha mtu kupitia upasuaji.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/DW

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman