1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Valls kumuunga mkono Macron

Sylvia Mwehozi
30 Machi 2017

Waziri mkuu wa zamani wa Ufaransa Manuel Valls siku ya Jumatano(29.03.2017) alitangaza kumuunga mkono mgombea wa urais Emmanuel Macron katika uchaguzi mkuu.

https://p.dw.com/p/2aJMf
Frankreich Paris Nationalversammlung Manuel Valls
Picha: Getty Images/AFP/A. Jocard

Valls anakuwa kiongozi wa juu wa kisosholisti kumgeuka mgombea wa chama chake na badala yake kumuunga mkono mgombea wa chama cha siasa za mrengo wa  kati.

Ingawa haikuwa dhahiri ikiwa uungwaji mkono huo wa Valls utamfaidisha Macron, ambaye kwa upole alimshukuru Valls, umeibua hasira miongoni mwa wasosholisti na uvumi wa vyombo vya habari juu ya mustakabali wa chama kikubwa cha mrengo wa kushoto.

Valls ambaye tangazo lake linakuja siku kadhaa baada ya mwanasiasa mkongwe msosholisti na waziri wa ulinzi Jean-Yves Le Drian kumuunga mkono Macron na kusema kwamba atafanya kila awezalo kuhakikisha kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen, aliye kwenye nafasi ya pili katika utafiti wa kura za maoni, kwamba hatochukua madaraka. Valls alipoulizwa ikiwa atampigia kura Macron amesema. "Ndio, kwasababu nafikiri huwezi kuiweka nchi katika hatari kwa hiyo nitampigia kura Emmanuel Macron, ninawajibika sio kwasababu ya moyo ni kwasababu ya kichwa," amesema Valls.

Frankreich Wahlen - Macrons Wahlkampf
Emmanuel Macron mgombea wa urais wa Ufaransa Picha: Getty Images/AFP/E. Feferberg

Kura za maoni za Ufaransa zinamwonyesha Macron kuwa mshindi wa urais katika raundi ya pili ya uchaguzi hapo Mei 7 ambapo atachuana vikali na Le Pen. Kura hizo zinamwonyesha mgombea wa kisosholisti Benoit Hamon anashika nafasi ya tano katika duru  ya kwanza ya mtoano hapo Aprili 23.

Hamon anayetaka kuhalalisha bangi na kutengeneza malipo ya serikali ya kila mwezi kwa kila mwananchi yupo katika nafasi ya kushinda asilimia 10 ya kura katika raundi ya kwanza kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Elable na kutolewa jana Jumatano.

Mgombea huyo ameukosoa uamuzi wa Valls na kutoa wito kwa wanasiasa wote wa mrengo wa kushoto kumuunga mkono huku zikiwa zimebaki siku 25 kabla ya raundi ya kwanza ya uchaguzi. "Ninatoa wito kwa wananchi wote wa mrengo wa kushoto kuwawekea vikwazo wale wanaotuchezea na ninawaomba kutowaunga mkono wanasiasa wasioamini chochote lakini zaidi wafuata upepo" amemalizia Hamon.

Frankreich Die Linke vor der Wahl | Hamon
Benoit Hamon mgombea wa urais nchini Ufaransa Picha: DW/D. Pundy

Hata hivyo Valls mwenyewe anasema chaguo lake halimaanishi kwamba atamfanyia kampeni Macron mwenye miaka 39 ambaye ni waziri mwenza katika serikali ya rais Francois Hollande kuanzia mwaka 2014 lakini aliyejiondoa mwaka jana kwa ajili ya kujiandaa na mbio za uchaguzi chini ya bendera yake kisiasa  En Marche.

Macron ambaye amejipatia uungwaji mkono wa wanasiasa wa pande zote za kulia na kushoto amesema hana nia ya kumjumuisha Valls katika serikali yake.

Taarifa hizo zimekuja siku moja baada ya mgombea anayewekwa katika nafasi ya tatu Francois Fillion aliyepo chini ya uchunguzi kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha kupata pigo zaidi baada ya mkewe raia wa Uingereza Penelope kuwekwa pia chini ya uchunguzi rasmi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Saumu Yusuf