1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo kutokana na virusi vya Corona vyapindukia 630

John Juma
7 Februari 2020

Watu 41 zaidi waliokuwa katika meli ya utalii ya Kijapani, wamebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona na hivyo kuongeza idadiya walioambukizwa ndani ya meli hiyo kufikia 61.

https://p.dw.com/p/3XP7s
China Wuhan Labor testet auf Coronavirus
Picha: AFP

Uchunguzi kuhusu virusi vya corona umebainisha kuwa watu wengine 41 waliomo kwenye meli ya utalii kwa jina Diamond Princess, pia wameambukizwa virusi hivyo, na hivyo kufanya idadi jumla ya walioambukizwa ndani ya meli hiyo kufikia 61. Meli hiyo ambayo imewabeba takriban watu 3,700, imewekwa kwenye karantini kwa muda wa wiki mbili sasa tangu ilipowasili katika bandari ya Yokohama, kusini mwa Tokyo, baada ya abiria mmoja aliyeshuka kwenye meli hiyo kugunduliwa kuwa na virusi hivyo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, watu 61 waliothibitishwa kuambukizwa ni miongoni mwa watu 272, ambao walipimwa kwa sababu walionyesha dalili za virusi hivyo au walikuwa karibu na abiria wa kwanza aliyeambukizwa.

Waziri wa Afya wa Japan Katsunobu Kato amewaambia waandishi wa habari kuwa watu 21 miongoni mwa 41 waliothibitishwa kuambukizwa ni raia wa Japan. Kato ameongeza kuwa uchunguzi zaidi utafanywa endapo abiria zaidi ndani ya meli hiyo wataonyesha dalili za kuugua.

Maafisa wa afya nchini Japan wameanza kuwaondoa wagonjwa kwenye meli hiyo kuwapeleka katika vituo vya afya.

​​​​Baadhi ya magari ya abiria yameonekana yakiwahamisha wagonjwa walioambukizwa kwenye meli ya utalii, na kuwapeleka katika vituo vya afya
​​​​Baadhi ya magari ya abiria yameonekana yakiwahamisha wagonjwa walioambukizwa kwenye meli ya utalii, na kuwapeleka katika vituo vya afyaPicha: picture-alliance/AP/The Yomiuri Shimbun

Idadi ya vifo nchini China kutokana na mlipuko wa virusi hivyo kwa sasa imepindukia watu 630, akiwemo daktari Li Wenliang aliyetoa tahadhari ya mwanzo kuhusu kitisho cha virusi hivyo. Hadi sasa, upande wa China bara pekee zaidi ya watu 31,120 wameambukizwa.

Virusi hivyo vimesambaa pia katika zaidi ya mataifa 20 ambako visa 260 vimethibitishwa.

Wanasayansi Hong Kong wavumbua kifaa cha kupima virusi vya corona

Hayo yakijiri, wanasayansi katika chuo kikuu cha Hong Kong wa sayansi na teknolojia wamesema wamevumbua kifaa cha kupima na kugundua kwa haraka virusi hivyo kwa wanadamu.

Wakitangaza hatua hiyo, wanasayansi hao wamesema duniani kote, changamoto kubwa imekuwa kubaini kwa haraka uwepo wa virusi hivyo mwilini.

Timu hiyo imesema kifaa walichokivumbua kinaweza kubaini virusi hivyo kwa muda wa dakika 40 pekee, tofauti na mfumo unaotumiwa sasa unaotumia kati ya saa moja na nusu hadi saa tatu.

Afisa wa afya akipima viwango vya joto vya abiria aliyewasili katika uwanja wa ndege wa Hong Kong
Afisa wa afya akipima viwango vya joto vya abiria aliyewasili katika uwanja wa ndege wa Hong KongPicha: Reuters/H. McKay

Wanasayansi kote duniani wanafanya juhudi kutafuta namna ya kutibu virusi hivyo vipya, ambavyo kwa sasa vinatishia kuwa janga la afya duniani.

Japan kuwazuia abiria wa meli kuingia

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ametangaza kuwa kuanzia Ijumaa, nchi yake haitawaruhusu abiria kutoka kwenye meli nyingine za utalii kuingia nchini humo, kama hatua ya kuepusha maambukizi zaidi nchini  Japan.

Idara ya usafiri wa angani nchini Italia pia imesema kuwa safari za kutoka na kwenda China zitaendelea kufungwa kutokana na virusi vya Corona

Nayo serikali ya Ujerumani inataka kuwahamisha raia wake wengine walioko Wuhan China. Hayo ni kulingana na gazeti la Der Spiegel.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ujerumani iliwahamisha raia 100 pamoja na familia zao kutoka Wuhan.

Vyanzo: RTRE, APE