1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vigogo wa kisiasa wawajibika Ujerumani

24 Septemba 2013

Siasa zimechemsha Ujerumani ambapo viongozi wa vyama mashuhuri vya kisiasa wa chama cha Free Democratic FDP wamejiuzulu na uongozi mzima wa chama cha Kijani kujizulu baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi.

https://p.dw.com/p/19mwu
Rainer Brüderle akiwa na Philipp Rösler.
Rainer Brüderle akiwa na Philipp Rösler.Picha: picture-alliance/AP Photo

Kiongozi wa chama cha FDP Phillip Rösler ametangaza kujiuzulu hapo Jumatatu baada ya chama chake kushindwa vibaya kuwahi kushuhudiwa kabla katika uchaguzi wa Ujerumani uliofanyika Jumapili na kusababisha kuenguliwa kwa chama hicho katika bunge la Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.

Rösler Naibu Kansela anayemaliza muda wake ambaye amejiuzulu kama kiongozi wa chama hicho chenye kupendelea wafanya biashara na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ni miongoni mwa mawaziri waliopoteza viti vyao katika uchaguzi huo ambapo chama chao kimeboronga vibaya.

Rösler mwenye umri wa miaka 40 ambaye alikuwa pia waziri wa uchumi katika serikali ya Merkel amesema wakati akijiuzulu kwamba huko ni kushindwa vibaya kabisa kwa chama hicho kuwahi kushuhudiwa katika historia.

Amekaririwa akisema "Bila ya shaka tumezungumzia juu ya mustakbali wa chama. Na kama niliyosema kwangu mimi mwenyewe binafsi huo ulikuwa ni ushindi mbaya kabisa wa chama.Nimeshika madaraka ya chama katika kipindi kigumu na juu ya kwamba kulikuwa na mafanikio fulani ya uchaguzi mwishowe hatukuweza kufanikiwa kuwa kitu kimoja na kushinda katika uchaguzi wa bunge na tayari nilikuwa nimesema kwamba nitawajibika."

Philipp Rösler kiongozi wa FDP.
Philipp Rösler kiongozi wa FDP.Picha: Reuters

Chama cha FDP ambacho mara nyingi kimekuwa kikishiriki katika serikali kama mshirika mdogo kuliko chama chengine chochote kile cha Ujerumani tokea kilipochaguliwa mara ya kwanza hapo mwaka 1949 kimeshindwa kujipatia asilimia tano ya kura ili kuweza kubakia bungeni.

Rösler na mgombea mkuu wa chama hicho Rainer Brüderle mwenye umri wa miaka 68 aliyeonekana kuwa na huzuni kubwa wote walikuwa tayari wametangaza hapo Jumapili kwamba watawajibika kisiasa kufuatia matokeo hayo ya uchaguzi.

Matumaini mapya ya FDP

Kijana anayawekewa matumaini mapya ya kuongoza chama hicho ni Christian Lindner mwenye umri wa miaka 34 katibu mkuu wa zamani wa chama hicho ambaye hivi sasa anakiongoza chama hicho katika jimbo la North Rhine Westphalia.Kiongozi huyo mpya atakuwa na majukumu ya kukiimarisha upya chama hicho ambacho bado kinaendelea kuwakilishwa katika mabunge kadhaa ya jimbo na kuwahi kuipatia Ujerumani mawaziri kadhaa mashuhuri wa mambo ya nje akiwemo Hans-Dietrich Genscher ambaye kwa kushirikiana na Kansela Helmut Kohl walisimamia kuungana upya kwa Ujerumani mbili hapo mwaka 1990.

Christian Lindner mjumbe wa kamati kuu ya chama cha FDP.
Christian Lindner mjumbe wa kamati kuu ya chama cha FDP.Picha: Reuters

Lindner yumkini akachaguliwa kuwa kiongozi mpya wa chama hicho katika mkutano mkuu wa chama utakaofanyika baadae mwaka huu na ameahidi hapo Jumatatu atapigania kurudisha heshima ya chama hicho.

Chama cha FDP ambapo wafuasi wake wanajulikana kama Waliberali pole pole kimekuwa kikibadili mwelekeo wake tokea kumalizika kwa Vita Baridi kutoka kuwa uliberali wa kisiasa hadi utetezi wa uhuru wa watu binafsi hadi kuwa uliberali wa kiuchumi na utetezi wa ubepari wenye kutegemea uhuru wa masoko.

Katika kipindi cha miaka minne iliopita chama hicho kimekuwa kwenye mfarakano wa ndani ya chama jambo ambalo linatajwa kuwa ndio lililosababisha kuanguka kwa chama hicho kwenye uchaguzi kutoka asilimia 10 iliokuwa ikishikilia tokea uchaguzi wa mwaka 2009 hadi kuwa asilimia 4.8 katika uchaguzi huu.

Uongozi mzima kujiuzulu

Wakati huo huo uongozi mzima wa chama cha Kijani cha watetezi wa mazingira umesema utajiuzulu kufuatia kupata pigo baya katika uchaguzi huo mkuu wa Ujerumani.Wenyeviti wenza wa chama hicho Cem Özdemir na Claudia Roth pamoja na baraza la kuu la chama hicho linaloongozwa na wagombea wakuu Jürgen Trittin na Katrin Göring-Eckart wataachia madaraka yao katika mkutano wao mkuu ujao wa chama wa katika kipindi hiki cha majira ya mapukutiko. Kwa mujibu wa Roth kujiuzulu huko kwa wajumbe sita wa Kamati Kuu ya Chama na wajumbe 16 wa baraza kuu la chama ni ishara kwa chama na wananchi kwa jumla kwamba viongozi wanawajibika.Miongoni mwa viongozi waandamizi wa chama hicho watakaojiuzulu ni pamoja na Renate Künast.

Uongozi wa chama cha Kijani (kutoka kushoto)Claudia Roth na Cem Ozdemir na wagombea wakuu wa uchaguzi Katrin Goering-Eckardt na Juergen Trittin.
Uongozi wa chama cha Kijani (kutoka kushoto)Claudia Roth na Cem Özdemir na wagombea wakuu wa uchaguzi Katrin Göring-Eckardt na Jürgen Trittin.Picha: picture-alliance/dpa

Akitangaza uamuzi huo Jumatatu Roth pia amesisitiza kwamba iwapo Kansela Angela Merkel atapendekeza kuunda serikali ya mseto na chama hicho pendekezo hilo linapaswa kuzingatiwa.
Kwa hivi sasa Merkel amewasiliana na chama kikuu cha upinzani SPD kupendekeza kile kinachojulikana kama serikali ya "muungano mkuu" na chama hicho.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu