1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vigogo wa SPD Wawashawishi Wanachama Shina

Oumilkher Hamidou29 Novemba 2013

Viongozi wa chama cha SPD wameanza kampeni kali ya kuwatanabahisha wanachama wake waunge mkono mkataba wa serikali ya muungano pamoja na vyama ndugu vya CDU na Christian Social Union-CSU.

https://p.dw.com/p/1AQUH
Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel anahutubia wafuasi huko HessenPicha: picture-alliance/dpa

Mara tu baada ya mkataba huo kutiwa saini alfajiri ya jumatano iliyopita wakuu wa chama hicho kikongwe kabisa cha kisiasa nchini Ujerumani wameingia njiani majimboni kuanza kuwatanabahisha wafuasi wao kuhusu umuhimu wa kuunga mkono mkataba huo wa kurasa 185, kura ya maoni ya wafuasi shina itakapoitishwa.Hadi december 14 ijayo matokeo ya kura hiyo ya maoni yatakapojulikana,jumla ya mikutano 150 itaitishwa ambapo makada wa chama hicho watafafanua yaliyofikiwa na kuelezea umuhimu wa kujiunga na serikali ya muungano wa vyama vikuu ,ambao baadhi ya wafuasi shina hawataki hata kuusikia.

Wana Social Democratic bado wanasumbuliwa na matokeo ya "muungano uliopita wa vyama vikuu" kati ya mwaka 2005 na 2009 ambapo chama chao kilijikuta kikipoteza zaidi ya asilio mia 10 ya kura uchaguzi mkuu ullipoitishwa mwaka 2009.

Matokeo December 14

Katika kampeni hizo zilizoanzia katika jimbo la Hessen mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel na vigogo wengine wa chama wamejitokeza kitu kimoja na kushadidia ridhaa walizozipata kutoka kambi ya bibi Angela Merkel,ikiwa ni pamoja na kiwango cha chini cha mishahara kwa wote.Wakuu wa tawi la vijana wa SPD-JUSOS ambao kijadi huelemea zaidi mrengo wa shoto nao pia wameingia njiani kuwatanabahisha wanachama.Mwenyekiti wa tawi hilo Sascha Vogt amekiri vijana wengi wana shaka shaka lakini anasema "watakapousoma mkataba huo na kuelewa kilichofikiwa wataukubali.

Koalitionsvertrag große Koalition CDU SPD 18. Legislaturperiode
VIongozi wa vyama vyote vitatu Angela Merkel wa CDU (kati) Horst Seehofer wa CSU (kulia) na Sigmar Gabriel wa SPD wakipeana mikono baada ya mkataba kutiwa sainiPicha: Reuters

Mbali na kiwango hicho cha mshahara,SPD wamefanikiwa kupata ridhaa katika madai ya kuzidishwa vitega uchumi katika sekta ya elimu na kupunguzwa makali sheria kuhusu uraia wa nchi mbili-watakaofaidika na hali hii mpya ni jamii ya wageni na hasa wa kituruki ambao kijadi hukipigia kura chama hicho cha Social Democratic.

Hata hivyo utaratibu huo wa kuulizwa wafuasi maoni yao katika kura ya maoni ambao ni wa kwanza wa aina yake nchini Ujerumani unatiliwa shaka na baadhi ya wadadisi kama unaambatana na muongozo wa katiba ya humu nchini.

Kuhusu hofu hizo,mwenyekiti wa SPd Sigmar Gabriel anasema::"Katika katiba imetejwa vyama vinabidi vizingatie maoni ya wananchi na nchini Ujerumani kuna sheria pia inayohusu vyama vya kisiasa na ambayo inahimiza kuwepo mfumo wa kidemokrasia ndani ya chama.Kwa hivyo sioni kwanini mfumo wa kidemkorasia usiruhusiwe chamani.Kinachofanywa na SPd ni cha maana na ni mfano pia wqa kuigizwa.Kwasababu watu wanajiunga na chama sio tu kwasababu ya kulipia ada bali pia wanataka kuwa na usemi."

Wengi wanaunga mkono

Matokeo ya kura ya maoni ya wanachama wa SPD kuhusu mkataba huo wa serikali ya muungano ya vyama vikuu yanatarajiwa kutangazwa December 14 ijayo.Pindi matokeo yake yakiwa "la" na idadi ya watakaoshiriki ikiwa chini ya asili mia 20,Angela Merkel anaweza kusaka muungano pamoja na walinzi wa mazingira die Grüne la sivyo uchaguzi mkuu mwengine utaitishwa.

Große Koalition CDU und SPD einigen sich 27. Nov. 2013 Koalitionsvertrag
VIongozi wa vyama hivyo vitatu na nyaraka za mkataba wa muunganoPicha: Reuters

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya umma uliochapishwa hivi punde na kituo cha pili cha televisheni cha humu nchini ZDF,asili mia 65 ya wananchi wa Ujerumani wanaunga mkono mkataba wa serikali ya muungano kati ya CDU/CSU na SPD.Na miongoni mwa wafuasi wa chama cha SPD asili mia 64 ndio wanaouunga mkono mkataba huo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu