1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana wawili wa kiyahudi washambuliwa Berlin

Oumilkheir Hamidou
18 Aprili 2018

Shambulio dhidi ya wayahudi lililotokea hadharani Berlin limezusha fadhaa na hasira Ujerumani. Watu 2 waliovaa vikofia vya wayahudi walitukanwa na kushambuliwa.Takwimu zinaonyesha hii si mara ya kwanza.

https://p.dw.com/p/2wHOO
Screenshot Youtube Antisemitischer Angriff in Berlin
Picha: Jüdisches Forum JFDA

Polisi mjini Berlin imesema vijana wawili  wenye umri wa miaka 21 na 24 waliokuwa wamevaa vikofia vya kiyahudi kichwani, walitukanwa na kushambuliwa hadharani na kundi la watu watatu wasiojulikana  wenye kuwachukia wayahudi, katika mtaa wa Prenzlauer Berg mjini Berlin.

Mmojawapo wa wahalifu hao alimpiga mikanda na baadae kwa chupa ya kigae kijana wa kiyahudi mwenye umri wa miaka 21. Mwenzake aliingilia kati na kuzuwia kwa namna hiyo hujuma zaidi dhidi ya kijana huyo wa kiyahudi.

Hujuma dhidi ya wayahudi zimeongezeka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita

Kwa mujibu wa kituo cha uchunguzi kinachokusanya maelezo kuhusu mashambulio dhidi ya wayahudi mjini Berlin, visa vya chuki dhidi ya wayahudi vimeongezeka kwa asili mia 60 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Kanda ya video iliyonaswa kwa simu ya mkononi ya mmojawapo wa wahanga hao wawili imeenea katika mtandao wa Facebook. Kanda hiyo inaonyesha jinsi watuhumiwa hao walivyokuwa wakimpiga mikanda na kumwita kwa kiarabu- "yahudi" kabla ya mtu mwengine kusitisha kunasa tukio hilo. Kanda hiyo ya video inaonyesha pia majaraha yaliyojaa katika mwili wa kijana huyo -majaraha yanayotokana na kupigwa mikanda. Polisi wanawatafuta ili kuwafungulia mashitaka watuhumiwa hao wasiojulikana.

Mshikamano kupinga chuki dhidi ya wayahudi katika mtaa wa Neuköln mjini Berlin
Mshikamano kupinga chuki dhidi ya wayahudi katika mtaa wa Neuköln mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa/Wolfgang Kumm

Ujerumani ina jukumu la kuhakikisha usalama wa wayahudi

Meya wa jiji la Berlin Michael Müller wa kutoka chama cha Social Democrat amelaani vikali shambulio hilo."Hisia za chuki dhidi ya wayahudi hazina nafasi katika mji tunaoishi wa Berlin amesema.

Waziri wa mambo ya nchi za nje Heiko Maas ameliambia shirika la mchanganyiko wa vyombo vya habari "Funke" tunanukuu" Si jambo linaloweza kuvumilika kuona  vijana watashambuliwa kwasababu tu wamevaa vikofia vya kiyahudi". Waziri Heiko Maas amesisitiza kwa kusema wajerumani wanajukumu la kudhamini usalama wa wayahudi wanaoishi humu nchini.

Waziri wa sheria Katarina Barley ambae sawa na waziri wa mambo ya nchi za nje Heiko Maas ni wanachama wa SPD, amezungumzia kuhusu "aibu kwa nchi yao."Ameshadidia watuhumiwa lazma wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Mwenyekiti wa baraza la wayahudi wa Ujerumani Joseph Schuster
Mwenyekiti wa baraza la wayahudi wa Ujerumani Joseph SchusterPicha: Imago/epd/H. Lyding

Mstari mwekundu umekiukwa

Mwenyekiti wa baraza la wayahudi nchini Ujerumani Josef Schuster amezungumzia kuhusu kukiukwa kwa mara nyengine tena mstari mwekundu. Anazitaka taasisi za sheria zidhihirishe kisa hicho hakikusababisha majaraha tu. Pindi watuhumiwa wakikamatwa, chanzo kinabidi kichunguzwe na kujulikana sababu zake. "Hakuna anaezaliwa na chuki dhidi ya wayahudi" amesema.

Kwa mujibu wa kituo cha utafiti na kukusanya maelezo kuhusiiana na visa vya chuki dhidi ya wayahudi-RIAS, kadhia 947 za chuki dhidi ya wayahudi zimeripotiwa  mjini Berlin katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, 18 kati ya visa hivyo ni mashambulio na 23 ni vitisho.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/epd/AP

Mhariri  Mohammed Abdul-Rahman