1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana Wetu - Mustakabali Wao

P.Martin5 Novemba 2007

Inatathminiwa kuwa takriban asilimia 20 ya vijana wanaishi kwa kutumia chini ya Dola moja kwa siku. Ni dhahiri kuwa,idadi ya vijana hao masikini ikiendelea kuongezeka,ni muhimu kuwajumuisha vijana hao katika sera za maendeleo duniani.

https://p.dw.com/p/C7rP

Vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ni robo ya umma wa kufanya kazi duniani lakini vijana ni nusu ya watu wasio na ajira.Hitilafu hiyo hasa yadhihirika katika nchi zinazoendelea na zile zenye maendeleo madogo,ambako kiasi ya asilimia 51 ya umma ni chini ya umri wa miaka 25.

Umoja wa Mataifa katika Malengo ya Maendeleo ya Milenia kwa ufupi MDG,umezindua ajenda ya kimataifa kukomesha umasikini kote duniani na hasa katika nchi zenye pato la chini kabisa na ambako kuna idadi kubwa ya vijana.Lakini hadi sasa,wajumbe vijana wanaohudhuria midahalo ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kila Septemba, kawaida hutoka nchi zilizoendelea na hasa kutoka Ulaya.

Sababu kuu ya kutopeleka wajumbe vijana, iliyotajwa na nchi zinazoendelea,ni gharama za usafiri na kuwaweka mjini New York majuma kadhaa. Nchi nyingi bado hazijatambua kuwa vijana wanaweza kusaidia kupata maendeleo.

Kwa mfano,Leticia Gasca wa Mexico alie na umri wa miaka 21,aliiwakilisha nchi yake katika Umoja wa Mataifa.Yeye,anafanya kazi pamoja na jamii za kienyeji na za mashambani,tangu alipokuwa na umri wa miaka 16.Miaka michache iliyopita,aliunda shirika lisilo la kiserikali,kuendeleza maendeleo sehemu za shambani.Anasema,alipokwenda Umoja wa Mataifa, alishiriki katika midahalo ya ushirikiano wa kitamaduni na dini kwa lengo la kuendeleza amani. Uzeofu aliopata umemtia moyo.

Lengo lake sasa ni kuendelea kushughulikia maendeleo ya vijijini na vijana.Vile vile anatazamia kuwa na tovuti kwenye mtandao wa Internet ili wajumbe vijana wa Mexico,waweze kubadilishana fikra zao pamoja na vijana wote duniani.

Mada zinazopewa umuhimu na Mradi wa Vijana wa Umoja wa Mataifa ni elimu,ajira,njaa,umasikini, afya na mazingira.Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa,wajumbe vijana hushiriki kwa mafanikio katika majadiliano yanayohusika na maendeleo endelevu,kuliko katika sekta nyingine.Vile vile vijana hufanikiwa kuzishawishi serikali kuwajibika zaidi.Si hilo tu,bali vijana sehemu mbali mbali duniani,hushughulikia miradi ya vijijini na husaidia kutekeleza malengo ya Umoja wa Mataifa.

Lakini kinachosikitisha ni kuwa tangu mwaka 2005 zaidi ya watoto milioni 113 wamenyimwa kusoma shule ya msingi na zaidi ya milioni 150 wala hawakumaliza elimu hiyo.Na hasa ni wasichana wanaonyimwa elimu ya shule ya msingi.Vile vile katika nchi zinazoendelea,kiasi ya watoto milioni 250 walio kati ya umri wa miaka 5 na 14 wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya kulazimishwa kufanya kazi.

Umasikini unaripuka kwa haraka kote duniani na ni vijana wanaothirika zaidi.Serikali zinapaswa kutambua thamani ya vijana na kugharimia miradi ya kuwasaidia vijana hao.