1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya amani vyapungukiwa fedha

P.Martin8 Desemba 2008

Vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa vinakabiliwa na mzozo wa fedha huku michango ikipunguka na wakati huo huo majeshi zaidi yakihitajiwa kila pembe ya dunia.

https://p.dw.com/p/GBQi

Tangu kuasisiwa kwa Umoja wa Mataifa hapo mwaka 1948,idara ya walinzi wa amani imekuwa kwa kasi-na bajeti yake imefikia Dola za Kimarekani bilioni 7.1 na hivyo kupindukia bajeti ya ofisi inayoendesha shughuli za umoja huo.

Kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Mataifa hata hiyo bajeti ya Dola bilioni 7.1 haitoshi,wakati umoja huo ukijiandaa kupeleka ujumbe nchini Somalia na kuzidisha huduma zake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,Sudan,Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati.Fabienne Hara alie Naibu-rais wa International Crisis Group lenye makao yake mjini Brussels Ubeligiji anasema,katika miaka michache ijayo,vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa huenda vikakabiliana na shida za fedha wakati ambapo nchi fadhila zimekumbwa na athari za mzozo wa fedha duniani.Anaonya,michango ya baadhi ya nchi huenda ikapunguka au ikasita kabisa.

Lakini hilo si tatizo pekee.Baadhi kubwa ya vikosi vya amani vya kama wanajeshi 112,000 walio kila pembe ya dunia,hutoka nchi zinazoendelea ambazo sasa zinasema zimeishiwa na wanajeshi wa kushiriki katika operesheni za kimataifa. Nchi za magharibi nazo zikilalamika kuwa hazitoweza kusaidia kwani tayari zinachangia Iraq na Afghanistan inahitaji vikosi ziada,zimetoa wito kwa nchi zingine kama vile Urusi kuchangia vikosi zaidi.

Ingawa ni nchi kama India na Pakistan zinazotoa mchango mkubwa wa wanajeshi,gharama za kuhudumia tume hizo hulipwa na mataifa tajiri.Kwa mfano Marekani peke yake hulipa kama robo ya bajeti ya vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa na si zaidi ya nchi kumi na mbili tajiri huchangia takriban asilimia tisini ya bajeti hiyo.Lakini sasa nchi hizo zote zinakabiliwa na kitisho cha uchumi unaozorota.

Vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa vinashiriki katika operesheni 63 kila pembe ya dunia.Kwa maoni ya wachambuzi na wanadiplomasia wa umoja huo,baadhi kubwa ya tume hizo zimefanikiwa.Lakini pia kuna makosa makubwa yaliyofanywa kwa sababu mbali mbali.Kwa mfano katika miaka ya tisini,vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa vilishindwa kuzuia mauaji ya halaiki nchini Rwanda na mauaji makubwa huko Bosnia.Wachambuzi wanasema,sababu mojawapo ni kupungukiwa fedha za kugharimia operesheni za kukabiliana na mizozo.

Na kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambako wakaazi laki mbili na nusu walikimbia makwao kwa sababu ya mapigano mapya yaliyozuka kati ya vikosi vya serikali na vya jenerali muasi Laurent Nkunda mashariki mwa nchi hiyo,maafisa wa Umoja wa Mataifa wamepuuza mawazo kuwa walinzi wa amani wangeweza kuzuia hali hiyo.Afisa mmoja amesema,wakati huo na hata hivi sasa hawana vikosi vya kutosha katika eneo hilo.Umoja wa Mataifa una wanajeshi 17,000 katika tume inayojulikana kwa jina la MONUC.Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha kupeleka wanajeshi na polisi 3,000 kuimarisha vikosi hivyo nchini Kongo.Lakini wana diplomasia wanasema,huenda ikachukua miezi kadhaa kabla ya kuweza kupata idadi hiyo.

Mchambuzi wa Kimarekani Max Bergmann wa Mtandao wa Usalama wa Taifa anasema,operesheni za Umoja wa Mataifa mara nyingine hazifanikiwi,lakini mara nyingi hayo ni matokeo ya kutokuwa na vikosi vya kutosha au kupungukiwa fedha.Umoja wa Mataifa unazidi kutegemewa kushughulikia maeneo ya matatizo na kuzuia migogoro kushika kasi.Lakini wakati huo huo michango ya fedha inapunguka.