1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Iraq vimefanikiwa kusogea hadi mto Tigris

Sylvia Mwehozi
9 Januari 2017

Vikosi maalum vya jeshi la Iraq vinavyopambana na kundi linalojiita Dola la kislamu IS vimeufikia ukingo wa mashariki katika Mto Tigris mjini Mosul

https://p.dw.com/p/2VV9z
Irak Mossul Militär
Picha: Getty Images/A.Al-Rubaye

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miezi mitatu tangu kuanza mashambulizi ya kuudhibiti tena mji huo ulio mikononi mwa wanamgambo ambao bado wanashikilia nusu nzima ya upande wa magharibi. 

Kundi la IS pia lilidai kuhusika na mojawapo ya mashambulizi mawili katika soko mjini Baghdad ambapo takribani watu 20 waliuawa, ikiwa ni shambulio la hivi karibuni katika mfululizo wa mabomu mbinu ambayo kwa hivi inatumiwa na kundi hilo wakati likizidi kupata shinikizo mjini Mosul ambako ni ngome yake ya mwisho nchini Iraq.

Kitengo cha kupambana na ugaidi CTS kimepigana na kufanikiwa kufika katika ukingo wa mashariki mwa mto Tigris. Hii inakuwa mara ya kwanza kwa vikosi vya Iraq katika mji huo kuufikia mto huo ambao unaigawa Mosul kati.

Irak US-Truppen in Mossul Lieutenant General Steve Townsend
Luteni Jenerali Steve Townsend, kamanda wa jeshi la muungano linaloongozwa na MarekaniPicha: Reuters/M. Al-Ramahi

Ingawa kikosi hicho hakitarajiwi kusonga mbele kwa kuuvuka mto kabla ya kudhibiti wilaya zote za mashariki, lakini uwepo wake katika mwambao huo unasemekana kuwa utawawia vigumu wanajihadi wa IS kusambaza silaha na wapiganaji kutoka upande mwingine.

Mwanajeshi mmoja wa kitengo cha tahadhari Kanali Hishamu Abdelkathem amenukuliwa akisema kuwa, "kwa haraka sana vikosi vyetu vilipoanza kusogea, safu ya ulinzi ya Daesh ilinza kudhoofika. wapiganaji wengi wamekimbia eneo hilo wakiacha vilipuzi, mikanda ya mabomu ya kujitoa mhanga na miili ya wale waliouawa. Mwanzoni walileta upinzani lakini tunashukuru Mungu vikosi vyetu vimeonyesha mafunzo yake kwa ubora na usahihi".

Licha ya kupiga hatua, vikosi hivyo pia vimekumbana na upinzani kutoka kwa wapiganaji wa IS katika eneo la kihistoria mashariki mwa Mosul, hayo ni kwa mujibu wa kamanda mmoja mwandamizi ikiwa ni jitihada za kuwafurusha kutoka vitongoji vya karibu.

Mamia ya raia wameyakimbia makazi yao karibu na Muthana ambako vikosi vya Iraq vilipashikilia siku mbili zilizopita kufutia mashambulizi ya usiku kucha.

Irak Region Mossul Irakiche Armee Zivilisten
Raia waliokimbia makazi yao Mosul wakipita karibu na wanajeshi wa IraqPicha: Reuters/T. Al-Sudani

Kwingineko mjini Baghad, mshambuliaji wa kujitoa mhanga aliwaua watu 13 wakati alipoendesha gari iliyotegwa vilipuzi katikati mwa soko la mboga katika wilaya inayokaliwa kwa wingi na Washia ya Jamila na kisha kuliripua.

Kundi la IS lilidai kupitia katika mtandao kuhusika na shambulio hilo na kusema lilikuwa likiwalenga "umati wa washia".

Saa chache baadae , mshambuliaji mwingine wa kujitoa mhanga aliyekuwa amevalia mabomu alijiripua mwenyewe katika soko lingine katika wilaya ya washia ya Baladiyat, na kuwaua watu saba kwa mujibu wa polisi.

Watu zaidi ya 80 wameuawa ndani ya kipindi cha wiki moja katika mashambulizi ya mjini Baghdad na miji mingine ya Iraq.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo