1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Lebanone vyapambana katika medani mbili.

Mohamed Dahman18 Juni 2007

Vikosi vya Lebanone leo hii vimekuwa vikiendesha mapambano katika medani mbili za mapambano dhidi ya wanamgambo wakiwasaka wapiganaji waliofyetuwa maroketi kwa Israel na kushambulia vikali kwa mizinga wanamgambo wa itikadi kali za Kiislam waliojichimbia kwenye kambi ya wakimbizi wa Kipalestina.

https://p.dw.com/p/CHCb
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa UNIFIL katika doriia kusini mwa Lebanon.
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa UNIFIL katika doriia kusini mwa Lebanon.Picha: AP

Vikosi vya Lebanone na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wako katika tahadhari kubwa kusini mwa Lebanone ikiwa ni siku moja baada ya kufyetuliwa kwa maroketi kwa Israel kwa mara ya kwanza tokea ipigane vita vya uharibifu mkubwa mwaka jana dhidi ya kundi la Kishia la Hizbollah nchini Lebanone.

Shambulio hilo katika eneo la Kiryat Shmona nchini Israel halikusababisha maafa yoyote yale isipokuwa uharibifu mdogo tu lakini limezidisha hali ya wasi wasi nchini Lebanone kufuatia miripuko kadhaa ya mabomu iliosababisha maafa nchini humo, mapigano na Waislamu wa itikadi kali wa Kisunni kaskazini mwa nchi hiyo na kuendelea kwa mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Magari ya deraya ya jeshi la Lebanone kadhalika yale ya Kikosi cha Muda cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanone UNIFIL yamekuwa yakipiga doria kwenye barabara inayokwenda sambamba na mpaka wa Israel.

Jeshi na polisi pia wameweka vituo vya ukaguzi katika eneo la mpaka ikiwa ni siku moja baada ya wanamgambo wasiojulikana kufyatuwa maroketi mawili kaskazini mwa taifa hilo la Kiyahudi.

Israel imesema Hizbollah hakihusika na shambulio hilo ambalo imelaumu kundi la Kipalestina bila ya kulitaja jina kwa kuhusika nalo.Hizbollah yenyewe pia imekanusha kuhusika.

Serikali ya Lebanone imeapa kuwasaka wahusika wa shambulio hilo na kikosi cha Umoja wa Mataifa UNIFIL kimelaani shambulio hilo kuwa ni ukiukaji wa mkubwa wa usitishaji wa mapigano ambao umekomesha mzozo wa Israel na Hizbollah.

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert ameelezea shambulio hilo la jana kuwa ni la wasi wasi sana na kusema kwamba yumkini likawa limetekelezwa na kundi la Al Qaeda au vuguvugu la Jihad kwa kutaka kuanzisha uchokozi ili kwamba kuondowa nadhari kwa yale yanayotokea Gaza.

Shambulio hilo la roketi limekuja baada kundi la Kiislam la Hamas kulin’gowa kundi la Fatah la Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina kutoka Ukanda wa Gaza ambao wenyewe umekuwa ukitumiwa kuvurumishia makombora hadi kusini mwa Israel.

Kaskazini mwa Lebanone jeshi limeendelea kuwashambulia kwa mabomu na mizinga wanamgambo wanaochochewa na Al Qaeda wa kundi la Fatah al Islam siku moja baada ya kusema kwamba wameteketeza vituo vya wanamgambo hao.

Vifaru na mizinga vimekuwa vikifyetuwa makombora kila baada ya dakika tano kwenye kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Nahr al Bared kaskazini wa mji wa Tripoli na kupiga majengo na kusababisha kuwaka kwa moto kwa maeneo kadhaa ya kambi hiyo.

Jeshi la Lebanone limesema kwamba limeingia ndani zaidi ya kambi hiyo tokea hapo Ijumaa na kuwarudisha nyuma wanamgambo hao hadi kusini ya kitongoji duni cha kambi hiyo.

Kundi la Fatah halikuweza kupatikana mara moja kuzungumzia hali hiyo.

Mapigano hayo yaliozuka hapo tarehe 20 mwezi wa Mei yameuwa watu 135,wakiwemo wanajeshi 68 na wanamgambo wa Kiislam 50.