1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya mchanganyiko kulinda amani Darfur

P.Martin12 Oktoba 2007

Nchi 16 zimetoa ahadi kwa Umoja wa Mataifa kuchangia wanajeshi au msaada wa miundombinu kwa ajili ya kikosi cha wanajeshi 26,000 wa umoja huo na Umoja wa Afrika.

https://p.dw.com/p/C7hr

Kikosi hicho,kinatazamiwa kulinda amani katika jimbo la mgogoro la Darfur,magharibi ya Sudan.

Baadhi kubwa ya majeshi hayo yatatumwa na nchi 10 za Kiafrika kama serikali ya Sudan ilivyotaka. Nchi hizo ni Burkina Faso,Misri,Ethiopia,Gambia, Ghana,Kenya,Malawi,Mali,Nigeria na Senegal.

Wanajeshi wengine watatoka Bangladesh,Jordan, Nepal na Thailand wakati Uholanzi na nchi za Scandinavia zikipeleka vikosi vya wahandisi na wauguzi.

Hata hivyo,Naibu Katibu Mkuu anaeshughulikia operesheni za kulinda amani,Jean-Marie Guehenno amesema,kunahitajiwa msaada wa dharura wa magari na helikopta za uchukuzi na za kijeshi,ili kuhakikisha kuwa vikosi vitaweza kwenda haraka katika maeneo ya migogoro.Akaeleza kuwa Darfur ni jimbo kubwa na wakaazi wake wametawanyika sehemu mbali mbali.Kwa hivyo,vikosi vitahitaji usafiri na nguvu za kijeshi ili kuweza kuhakikisha ulinzi wa raia hao.

Kwa upande mwingine,mauaji ya walinzi 10 wa amani wa Umoja wa Afrika hayakuhatarisha tu mkutano wa amani uliopangwa kufanywa tarehe 27 Oktoba nchini Libya bali ujumbe wa vikosi vya amani pia umetiwa mashakani.Kwani ripoti zinasema,Senegal imetishia kuondosha majeshi yake kufuatia mauaji hayo.

Mnamo mwezi Julai,Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,kwa kauli moja liliidhinisha kuunda kikosi cha mchanganyiko cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kulinda amani Darfur.Kikosi hicho cha 26,000 kinatazamiwa kuwa na wanajeshi 19,000, zaidi ya polisi 600 na wafanyakazi wa kiraia wapatao kama 5,500.Huo utakuwa ujumbe mkubwa kabisa,baada ya tume ya Umoja wa Mataifa ya 17,000 nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Kikosi hicho kipya cha mchanganyiko,kitajumuisha tume ya Umoja wa Afrika iliyopo Darfur hivi sasa.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa,mgogoro wa Darfur umesababisha vifo vya zaidi ya watu 200,000 na wengine milioni 2.5 wamepoteza makaazi yao.