1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Syria vyapelekwa Manbij

Sekione Kitojo
28 Desemba 2018

Jeshi la Syria  limesema  limeweka  vikosi vyake katika  mji  wa Manbij kaskazini magharibi mwa nchi hiyo leo Ijumaa, baada  ya wanamgambo wa Kikurdi wa kundi la YPG kuitaka serikali ya mjini Damascus kuulinda mji huo.

https://p.dw.com/p/3AjmS
Syrien | Free Syrian Army (FSA) auf dem Weg zur Front in Manbij
Picha: Getty Images/Anadolu Agency/H. el Homsi

Hatua  hiyo  imekuja  kutokana  na  kitisho cha  mashambulizi kutoka  majeshi ya  Uturuki huku  nchi  hiyo  ikipinga  hatua  hiyo  iliyochukuliwa  na   wanamgambo  hao.

Uturuki  imesema  leo kwamba wanamgambo  wa  Kikurdi  nchini Syria  hawana  haki  ya  kuomba  msaada   kutoka  serikali  ya  Syria kupambana  na  kitisho  hicho  cha  mashambulizi  kutoka  Uturuki upande  wa  kaskazini.

Wanamgambo  wa  kundi  lijiitallo Vikosi  vya  Ulinzi  wa  Umma, YPG, vinavyodhibiti  eneo  hilo kwa  silaha  hawana  haki  ama nguvu  za  kutoa  taarifa  ya  kukaribisha  makundi mengine  kwa niaba  ya  watu  wa  eneo  hilo, imesema  wizara  ya  ulinzi  ya Uturuki.

Syrien | Free Syrian Army (FSA) auf dem Weg zur Front in Manbij
Magari yenye silaha ya kikosi cha Hamza chenye mafungamano na jeshi la Syria vikielekea katika mji wa ManbijPicha: Getty Images/Anadolu Agency/H. el Homsi

Vikosi  vya  serikali  ya  Syria  vilivyopelekwa  katika  eneo  la Manbij  vimeingia  katika  mji  wa  Manbij  kwa  mujibu  wa  msemaji wa  jeshi  la  Syria  brigedia  jenerali  Ali Mayhoub.

"Taarifa ya mamlaka  kuu  ya  jeshi  la  Syria, kwa  misingi ya  jeshi la ulinzi  na dhamira  yake  ya  jumla  kuhusiana na  jukumu  la utekelezaji wa  ulinzi  wa  kila  sehemu  ya mipaka ya  jamhuri  ya Syria, na  kujibu  miito ya  watu  wa  Manbij, majeshi  ya  ulinzi yametangaza  kwamba wapiganaji  wa  jeshi  ya  Syria  wameingia Manbij na  kupandisha  bendera ya  jamhuri  ya  Kiarabu  ya  Syria."

Syria yapeleka  majeshi  Manbij

Shirika  linaloangalia  haki  za  binadamu  nchini  Syria, lenye  makao yake  makuu  nchini  Uingereza, limesema  majeshi  ya  serikali yamewekwa  nje  ya  mji  huo, kati ya  mji   huo  na  eneo  ambalo liko  katika  ushawishi  wa  Uturuki.

Uamuzi  wa  ghafla  wa  rais  wa  Marekani  Donald Trump kuviondoa  vikosi  vya  jeshi  la  nchi  hiyo  kutoka Syria  kumewatia shaka  wapiganaji  wanaoongozwa  na  Wakurdi  ambao wamepambana  na   kundi  linalojiita  dola  la  Kiislamu  pamoja  nao kwa  miaka  kadhaa.

Syrien US Armee in Manbij
Wanajeshi wa Marekani wakipewa maelekezo kabla ya kufanya doria pamoja na wanajeshi wa Uturuki mjini ManbijPicha: -picture alliance/AP Photo/Z. Garbarino

Viongozi  wa  Wakurdi  wanahangaika  kupata  mkakati  wa  kule kulilinda  jimbo  lao  ambalo  limesambaa katika  maeneo  ya kaskazini  na  mashariki, ambako  kuwapo  kwa  wanajeshi  2,000 wa Marekani kumezuwia  hadi  sasa  mashambulizi  ya  Uturuki, ambayo inawaangalia  wapiganaji  wa  Kikurdi  kuwa  kitisho  kwa  maeneo yao  na  imeapa  kuwamaliza.

Mji  huo  unashikilwa  na  baraza  la  kijeshi  la  manbij, wapiganaji wenye  mafungamano  na  kundi  la jeshi  la  Syria, wanapakana  na maeneo  yanayoshikiliwa  na  waasi  wanaoungwa  mkono  na Uturuki  ambao  wamekuwa  wakijitayarisha  kwa  mashabulizi.

Mwandishi: Sekione  Kitojo/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef