1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia: Tigray yarusha maroketi kuulenga mji wa Bahir Dar

Daniel Gakuba
20 Novemba 2020

Wanajeshi wa mkoa wa Tigray wameshambulia kwa roketi mji wa Bahir Dar mkoani Amhara, lakini taarifa zinaarifu kuwa hakuna aliyeuawa. Wakati huo huo vikosi vya serikali kuu vinazidi kuukaribia mji mkuu wa Tigray, Mekelle.

https://p.dw.com/p/3lbPS
Äthiopien Amhara grenze zu Tigray | Militäreinheiten der TPLF
Wanajeshi wa vikosi vya Tigray wakielekea mstari wa mbele wa mapiganoPicha: Tiksa Negeri/REUTERS

Ofisi ya msemaji wa serikali ya mkoa wa Amhara imetangaza kupitia mtandao wa facebook kuwa shambulizi kutoka chama tawala mkoani Tigray, TPLF limefanyika usiku wa manane kuamkia leo, na kwamba halikusababisha madhara yoyote. Hayo yamethibitishwa na mwandishi kutoka eneo hilo, ambaye amelithibitishia shirika la habari la Reuters kuwa amesikia miripuko miwili, na kuongeza kuwa eneo la shambulio hivi sasa limewekewa vizuizi.

Soma zaidi: Vikosi vya Ethiopia vyaukomboa mji mwingine mkoani Tigray

Mtu mwingine aliyesema ameisikia pia miripuko miwili, amearifu kuwa habari zilizopo ni kwamba maroketi hayo yalianguka karibu na uwanja wa ndege.

Äthiopien Konflikt Tigray | Grenzstadt Sudan al-Fashqa, Flüchtlinge
Watoto ni miongoni mwa watu wanaotaabika makambiniPicha: El Tayaeb Siddig/REUTERS

Wiki iliyopita, wanajeshi wa TPLF walivishambulia kwa maroketi viwanja viwili vya ndege katika mkoa wa Amhara, na kuulenga pia uwanja wa mji mkuu wa nchi jirani ya Eritrea.

Mkoa wa Amhara umetuma vikosi vyake vya kijimbo kupigana bega kwa bega na jeshi la serikali kuu dhidi ya waasi wa mkoani Tigray.

Mji wa Mekelle katika kilengeo

Hapo jana serikali ya shirikisho ya Ethiopia ilisema katika ripoti kuwa inaukaribia mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekelle, ambao viongozi wa jimbo hilo walioasi wamesema wanafanya kila juhudi kuulinda.

Mzozo huu wa ndani wa Ethiopia umesababisha maafa makubwa ya kibinadamu. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Watoto, Unicef, watoto milioni 2.3 katika eneo la mapigano wameachwa bila huduma za msingi, na maelfu wengine wanakabiliwa na kitisho katika kambi za wakimbizi.

Soma zaidi: Gutteres atoa wito wa kusitishwa mapigano Tigray, Ethiopia

Mamia ya watu wamekwishauawa katika mapigano hayo, na maelfu wamelazimika kuyapa kisogo makaazi yao na kukimbilia nchini Sudan kuyanusuru maisha yao.

Äthiopien I Situation in der Region Tigray
Wapiganaji wa mkoa wa Amhara waliojihami kwa vitaPicha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Dhiki kwa waliohamia makambini

Maisha katika kambi hizo, kama anavyoeleza mkimbizi huyu kutoka Tigray aliyejitambulisha kwa jina la Almas, ni magumu.

''Tulipofika hapa, kitu pekee tulichokikuta ni maji. Hakukuwepo chakula, dawa, madaktari wala magari ya kubeba wagonjwa'', amesema Bi Almas na kuongeza kuwa watu wanapougua wanaomba kuhamishwa, lakini hilo haliwezekani kwa sababu hakuna magari ya wagonjwa wala dawa.

Soma zaidi: Mvutano wa nchini Ethiopia

Chama cha TPLF kiliitawala Ethiopia kwa miongo kadhaa kama kundi lenye nguvu zaidi katika muungano wa vyama vya kikabila hadi waziri mkuu wa sasa Abiy Ahmed alipochukuwa madaraka mwaka 2018, baada ya vuguvugu la maandamano lililoambatana na umwagikaji wa damu.

Tangu wakati huo, Abiy ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel amewaachia maelfu ya wafungwa wa kisiasa kutoka gerezani, na kuwasimamisha kizimbani maafisa wengi wa serikali iliyomtangulia.

Watu wa jamii ya Tigray wanamtuhumu kuwaandama na kuwafukuza kutoka nyadhifa muhimu za uongozi, shutuma ambazo serikali inazikanusha.

 

rtre,afpe