1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Ukraine vyakaribia Donetsk

Admin.WagnerD5 Agosti 2014

Ukraine imesema kuwa vikosi vyake vinakaribia kuingia kwenye ngome kuu inayoshikiliwa na waasi katika mkoa wa Donetsk na imewataka wapiganaji kuwaachia raia ili kuyakimbia mapigano katika miji ya mashariki.

https://p.dw.com/p/1CozY
Vikosi vya Ukraine vikiwa katika operesheni
Vikosi vya Ukraine vikiwa katika operesheniPicha: Reuters

Msemaji wa usalama wa taifa nchini Ukraine, Andriy Lysenko, amesema vikosi vya Ukraine kutoka kitengo cha kupambana na ugaidi, jana viliutwaa mji wa Yasinuvata, ulioko umbali wa kilomita 19 kaskazini mwa Donetsk, ambao ni njia muhimu ya reli.

Amegusia kuwa mandaalizi ya kuuushambulia mji huo yanaendelea, ingawa hakutoa taarifa zaidi, wakati ambapo hofu ya kuzuka kwa mzozo wa kibinaadamu ikiongezeka.

Hatua ya mji huo kudhibitiwa, imesababisha Donetsk kuzingirwa kuanzia kaskazini na pia kufungwa kwa njia muhimu iliyokuwa inasaidia kusambaza silaha na teknolojia kwa magaidi.

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, vikosi vya serikali ya Ukraine vilifanikiwa kuingia katika eneo la mashariki na vinakaribia kuwasambaratisha wapiganaji wa Donetsk kutoka kwenye mpaka wa Urusi na washirika wao wa Lugansk, mji wa pili kwa ukubwa, unaoshikiliwa na waasi.

Wakati hayo yakijiri, Ukraine inafanya mazungumzo na Urusi kuhusu kurejeshwa zaidi ya wanajeshi 300 wa Ukraine waliovuka mpaka kuingia Urusi, wakati wakipambana na waasi.

Urusi kusaidia kurejeshwa wanajeshi wa Ukraine

Akizungumza kwenye televisheni ya Urusi, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Sergei Lavrov amesema Urusi itasaidia kuwezesha kurejeshwa wanajeshi hao.

Hata hivyo, idara ya usalama ya Urusi imesema walinzi wa mpakani wamewaruhusu raia 438 wa Ukraine kuvuka mpaka wa Gukovo, ulioko kati ya mji wa Luhansk na Rostov, baada ya kukubali kusalimisha silaha.

Wanajeshi wa Ukraine wakifanya mashambulizi
Wanajeshi wa Ukraine wakifanya mashambuliziPicha: picture-alliance/dpa

Katika hatua nyingine, Urusi imetangaza kuanza mazoezi mapya ya kijeshi yatakayozishirikisha ndege 100 za kivita kwenye eneo lake la kusini.

Aidha, Urusi huenda ikaweka vikwazo au kuzizuia ndege za mashirika ya Ulaya zinazotumia njia ya Trans-Siberia, baada ya Umoja wa Ulaya kuweka vikwazo kwa Ukraine.

Gazeti la kila siku la Vedomosti, limeripoti kuwa ndege ya Dobrolyot inayomilikiwa na shirika la taifa la Aeroflat, ilifuta safari zake zote za ndege wiki iliyopita, kwa sababu Umoja wa Ulaya uliongeza vikwazo kwenye ndege zinazokwenda Crimea, eneo lililojitenga na Ukraine mwezi Machi mwaka huu.

Wakati huo huo timu ya wataalamu wa kimataifa imeanza tena uchunguzi katika eneo ilikoangushwa ndege ya Malaysia chapa MH17, kwenye eneo linaloshikiliwa na waasi. Watu wote 298, wengi wao wakiwa raia wa Uholanzi, waliuawa katika ajali hiyo ya Julai 17, na hadi sasa majeneza 220 yamesafirishwa kwenda Uholanzi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,DPAE
Mhariri: Josephat Charo