1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya UN vimefanikiwa kuzuia jaribio la shambulizi DRC

Saumu Mwasimba
9 Desemba 2019

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO, kimesema wanajeshi wake wamezuia jaribio la shambulizi kwenye kambi ya Biakato, katika jimbo la Ituri.

https://p.dw.com/p/3USQe
Demokratische Republik Kongo | Überfall auf UN-Lager in Beni
Picha: Reuters/File Photo/O. Oleksandr

Vikosi vya Umoja wa Mataifa vimefanikiwa kuzuia jaribio la shambulizi katika moja ya kambi zake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Kikosi cha kulinda amani cha umoja huo nchini Kongo, MONUSCO kimesema kuwa wanajeshi wake walizuia jaribio hilo kwenye kambi ya Biakato, katika jimbo la Ituri usiku wa kuamkia jana.

MONUSCO imesema hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa. Eneo la mashariki mwa Kongo limekuwa likishambuliwa kwa miaka sasa na wanamgambo wanaothibiti maeneo ya kadhaa nchi hiyo.

Mwishoni mwa mwezi Oktoba, jeshi la Kongo lilianzisha operesheni dhidi ya kundi la wanamgambo la ADF. Katika kujibu mashambulizi ADF imefanya mauaji katika juhudi za kuwakatisha tamaa raia kulisaidia jeshi hilo.

Maandamano yameibuka kwenye mji wa mashariki mwa Kongo, Beni, ambako wakaazi wake wanaishutumu MONUSCO kwa kushindwa kuwalinda dhidi ya ADF. Kiasi cha watu wanane wameuawa katika maandamano ya kuipinga MONUSCO tangu Novemba 23.