1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Uturuki vyaendeleza mashambulizi Syria

John Juma
10 Oktoba 2019

wizara ya ulinzi nchini Uturuki imesema mashambulizi ya ardhini na angani yameendelea usiku kucha kuwalenga wanamgambo wa Kikurdi na maeneo yao nchini Syria.

https://p.dw.com/p/3R1gG
Syrien Konflikt Grenze Türkei | Türkischer Panzer
Picha: picture-alliance/Zuma Press/Turkish Defense Ministry

Wizara ya ulinzi nchini Uturuki imesema vikosi vyke vinavyofanya mashambulizi ya kijeshi kaskazini mashariki mwa Syria vimekamata maeneo yaliyolengwa na kwamba operesheni hiyo iliyoanza jana inaendelea vyema. Hii leo, Baraza la usalama la  Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana kuijadili Syria.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, wizara ya ulinzi nchini Uturuki imesema mashambulizi ya ardhini na angani yameendelea usiku kucha kuwalenga wanamgambo wa Kikurdi, kundi ambalo Uturuki inachukulia kuwa la kigaidi.

Wizara hiyo imesema ndege na magari ya kivita ya Uturuki yamefanya mashambulizi 181 mashariki mwa mto Euphrates ndani ya Syria tangu walipoanza mashambulizi jana.

Operesheni hiyo ilianza  baada ya Marekani kuwaondoa wanajeshi wake katika eneo hilo. Katika mpaka wa kaskazini mwa Syria, wakaazi waliingiwa na hofu na wasiwasi, wengine wakijaribu kukimbilia usalama kwa miguu na wengine kwa magari.

Uturuki inapoyashambulia maeneo ya Wakurdi wa YPG nchini Syria na kusogea zaidi mashariki mwa mto Euphrates; katika mji wa Diyarbakir ambao wengi wa wakaazi wake ni Wakurdi kusini mashariki mwa Uturuki, Wakurdi wametaka kuwe na amani. Mahmut Ozkan ambaye ni mmoja wa wakaazi wa Diyarbakir amesema:

Mwanamke akibeba vitu vyake kichwani huku akikimbilia usalama baada ya vikosi vya Uturki kuanza mashambulizi kaskazini mashariki mwa Syria.
Mwanamke akibeba vitu vyake kichwani huku akikimbilia usalama baada ya vikosi vya Uturki kuanza mashambulizi kaskazini mashariki mwa Syria.Picha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

"Sababu za Uturuki kushambulia zinapaswa kuchunguzwa. Kwa nini waliingia Syria? Kwa nini mazingira yalitengenezwa hili lifanyike? Mtu anapaswa kujiuliza maswali haya. Mimi napendelea amani. hali mbaya ya amani  ni bora zaidi kuliko vita bora.

Operesheni hiyo imekosolewa kiasi kikubwa ulimwenguni.

Kutokana na aibu ya jukumu la Marekani kuiachia Uturuki kufanya mashambulizi Syria, baadhi ya wakuu wa chama tawala cha rais wa Marekani Donald Trump wamemshutumu kwa kuwaacha Wakurdi wa Syria, ambao wamekuwa watiifu kwa Marekani katika vita dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS.

Jumuia ya kujihami ya NATO imesema inadhamiria kuweka ‘eneo salama, ili kuwarudisha mamilioni ya wakimbizi wa Syria. Lakini mataifa yenye nguvu kubwa ulimwenguni yanahofia hatua ya Uturuki inaweza ikazidisha machafuko na inaweza kuruhusu wafungwa wa IS kutoroka.

Rais Donald Trump ameyataja mashambulizi ya Uturuki kuwa hatua mbaya na amekana kuyaidhinisha. Trump amesema alitarajia Uturuki kuwalinda raia na waumini walio wachache na izuie kutokea kwa mzozo wa kibinadamu, kama ambavyo Uturuki ilisema.

Vikosi vya upinzani Syria vinavyoungwa mkono na Uturuki vikiingia eneo la Tel Abyad kuelekea Syria.
Vikosi vya upinzani Syria vinavyoungwa mkono na Uturuki vikiingia eneo la Tel Abyad kuelekea Syria.Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Hii leo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana kujadili mzozo wa Syria, kufuatia ombi la Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji na Poland ambao ni wanachama wake kutoka Ulaya.

Kundi linaloongozwa na Wakurdi pamoja na wanaharakati wa Syria limedai kuwa licha ya mashambulizi makali ya mabomu ambayo yamefanywa na Uturuki, vikosi vya Uturuki havijapiga hatua kubwa katika maeneo waliyohama tangu mashambulizi yaanze. Hata hivyo madai yao yasingeweza kuthibitishwa.

Maafisa wa Kikurdi na Marekani wamesema kwamba hii leo, Wakurdi wamesitisha operesheni zao zote dhidi ya kundi la IS, ili kukabili vikosi vya Uturuki vinavyoendelea kusogea ndani zaidi ya Syria.

Mustafa Bali ambaye ni msemaji wa vikosi vya Kikurdi nchini Syria (Syria Democratic Forces) SDF  amesema wapiganaji wao wamewashambulia na kuwafukuza wanajeshi wa ardhini wa Uturuki.

Uturuki imesema inalenga kuweka ‘eneo salama' ambalo litawafukuza wanamgambo wa Kikurdi mbali na mpaka wake kisha wakimbizi milioni 2 wa Syria waweze kurudisha eneo hilo.

Vyanzo: APE, RTRE