1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vilabu 3 vya England kucheza fainali

24 Mei 2021

Timu tatu za England zitakuwa zinacheza fainali za mashindano ya Ulaya wiki hii, Manchester United wakiwa wanaingia uwanjani Jumatano kupambana na Villareal ya Uhispania kwenye fainali ya Europa League.

https://p.dw.com/p/3tsWm
Fussball I Premier League I Manchester United v Fulham
Picha: Laurence Griffiths/REUTERS

Jumamosi Manchester City watakuwa wanapambana na Chelsea yake Thomas Tuchel kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Manchester United watakuwa wanaingia uwanjani hapo keshokutwa Jumatano kucheza na Villareal huko Gdansk, Poland na United huenda wakamkosa beki wao muhimu na nahodha Harry Maguire kwa fainali hiyo kama anavyoeleza hapa kocha wao ole Gunnar Solksjaer.

"Bila shaka anataka kucheza. Itategemea na daktari atakavyozungumzia hali yake ila kama nilivyosema, sitarajii awe tayari. Haonekani kuwa katika hali nzuri ila ninasalia kuwa na matumaini," alisema Solksjaer.

Manchester City nao watakuwa wanataka kulipiza kisasi cha kufungwa na Chelsea katika nusu fainali ya FA Cup watakapopambana Jumamosi huko Ureno katika uwanja wa Estadio do Dragao. City ndio wanaopigiwa upatu kunyakua ubingwa huo wa Ulaya na iwapo watafanya hivyo basi itakuwa ni mara ya kwanza kabisa katika historia yao. Huyu hapa kocha wao Pep Guardiola aliyekuwa akizungumza baada ya timu yake kukabidhiwa kombe la ubingwa wa England Jumapili.

UEFA Champions League I Chelsea v Real Madrid Thomas Tuchel
Kocha wa Chelsea Thomas TuchelPicha: Glyn Kirk/AFP

"Tulifurahia wiki mbili zilizopita, sisi ni mabingwa na leo tunasherehekea. Kesho tuko mazoezi, keshokutwa ni mapumziko na baada ya hapo tutakuwa na siku mbili za maandalizi ya fainali ya Champions League, kisha tuingie uwanjani," alisema Guardiola.

Kocha wa Chelsea Thomas Tuchel anasema timu yake ilikuwa na bahati jana kwani nusra waikose nafasi ya Cahmpions League msimu ujao baada ya kufungwa na Aston Villa.

"Tuna bahati kwamba Tottenham walitumalizia kazi leo, lakini Jumamosi tunastahili kuwa makini na kutumia nafasi zetu iwapo tunataka kupata matoeko mazuri katika mechi hiyo," alisema Tuchel.