1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi Kenya wasisitiza amani.

Lilian Mtono
27 Novemba 2019

Viongozi wametoa wito wa amani na umoja katika taifa lenye uchumi mkubwa katika kanda ya Afrika Mashariki ili taifa la Kenya listawi, wakati wakizindua ripoti ya Jopo la Maridhiano BBI.

https://p.dw.com/p/3Tq8F
Kenia Präsidentschaftswahl Wahlsieger Uhuru Kenyatta
Picha: Reuters/T. Mukoya

Viongozi hao wamewataka wanasiasa kutotumia hafla ya leo kuunda miungano ya kisiasa taifa linapoelekea kwenye uchaguzi na badala yake kuunganisha Wakenya. Rais Uhuru Kenyatta aliongoza hafla hiyo ya kitaifa.

Kenyatta akabiliwa na uasi wa kisiasa katika ngome yake

Kwa mara ya kwanza kwa kipindi kirefu katika siasa za taifa viongozi wa upinzani waliketi kwenye meza duara na viongozi wa serikali na hata kupatiwa nafasi ya kuhutubia zaidi ya wajumbe 4000 pamoja na mabalozi waliokongamana katika ukumbi wa Bomas. Kongamano hilo ni ishara kuwa viongozi wanataka mwanzo mpya wa taifa lenye umoja licha ya tofauti zao kisiasa na kikabila.

Ripoti ya BBI inaelekea kuwa imekubaliwa na vyama mbali mbali vya kisiasa kulingana na wawakilishi waliohutubia, hata hivyo itahitaji kupigwa msasa. Akiizindua ripoti hiyo rais Uhuru Kenyatta alihutubia zaidi ya saa moja huku akiwataka Wakenya kufahamu kuwa ripoti yenyewe haikuundwa kwa maslahi ya wachache bali kwa manufaa ya Wakenya wote.

Kenia Uhuru Kenyatta  William Ruto
Rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto katika picha ya pamoja baada ya kutangazwa washindi kwenye uchaguzi wa marudio wa urais, mwaka 2017Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Ripoti hiyo sasa inafungua ukurasa mpya wa mustakabali wa taifa ambao huenda ukaathiri siasa za urithi na siasa za uchaguzi mkuu ujao mwaka 2022. Jopo la maridhiano kwenye ripoti hiyo lililenga kujenga Kenya thabiti yenye umoja na kuzuia maafa na vurugu ambazo hushuhudiwa kila baada ya miaka mitano. Hata hivyo ni ujumbe wa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kupitia waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi uliobadilisha mazingira na kuziteka nyoyo za wakenya ambao mara nyingi hujificha kwenye vyandarua vya kikabila, wakati wa uchaguzi.

Palamagamba amewaonya viongozi hao kuhakikisha wanaodoa tofauti zilizojikita kwenye tofauti za kikabili ili kuwaepusha wananchi wao na madhila yanayojitokeza mara kwa mara, haswa wakati wa uchaguzi na kusababisha majanga makubwa.

Kenia Oppositionsführer Raila Odinga
Raila Odinga, amewaonya Wakenya kuikubali ripoti hiyo, kwani ni ya maslahi ya ummaPicha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye amewania urais mara nne bila ya ufanisi alilipongeza jopo hilo kwa kazi ya kuyakusanya maoni ya Wakenya. Ujio wake na ukaribu wake na rais Kenyata serikalini katika siku za hivi karibuni umekitikisa chama cha Jubilee na hata kutishia kukigawanya huku wafuasi wa naibu rais William Ruto mara nyingi wakimsuta, suala ambalo rais Kenyatta alilipuuzilia. Lakini uhusiano wake na serikali umeyeyusha uwezo wa upinzani kuikosoa serikali.

Rais kuhudumu kwa miaka saba Kenya - ripoti

Kuhusiana na ripoti hiyo, Odinga, amezidi kuwasisitiza Wakenya kuikubali kwa kuwa haikuandaliwa kwa maslahi yake, na kusema kwamba kuna wakati ataondoka na kuiacha ripoti hiyo.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita ripoti ya BBI, imekuwa ikiibua mijadala kwenye majukwaa ya kisiasa huku ikiligawanya taifa kwa makundi yanayomuunga mkono Rais Kenyatta na Raila Odinga na upande mwingine naibu rais William Ruto. Lakini aliposimama kuhutubia naibu rais aliashiria msimamo tofauti kinyume na injili ya siasa ya wafuasi wake.

Mara nyingi wanasiasa wameonekana kuwa vigeugeu, wakizungumza hivi leo lakini matendo yao yanakuwa tofauti, kesho. Je, kwa kipindi kijacho mirindimo ya siasa katika taifa la Kenya, itanyamazishwa na ripoti ya BBI?

Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi