1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika wataka ahadi zitimizwe

Mwadzaya, Thelma7 Julai 2008

Kikao cha mataifa manane yaliyostawi kiviwanda ulimwenguni G8 kinaendelea mjini Toyako kaskazini mwa Japan.Mkutano huo wa siku tatu unawaleta pamoja wajumbe zaidi ya alfu 2

https://p.dw.com/p/EXqH
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Japan Yasuo Fukuda katika kikao cha TokayoPicha: AP

Viongozi wa Afrika wanatoa wito kwa kundi la G8 kukabiliana na ongezeko la bei za mafuta na chakula na kuonya kuwa matatizo hayo huenda yakachagiza hali mbaya zaidi barani Afrika.

Wito huo umetolewa wakati viongozi wa kundi la mataifa manane yaliyostawi kiviwanda G8 wakianza rasmi mkutano wao wa kila mwaka kisiwani Hokkaido kaskazini mwa Japan.Viongozi 7 wa bara la Afrika nao walishiriki katika kikao maalum pamoja na viongozi wa G8.

Polisi wa kupambana na vita waliojihami kwa ngao waliwazuia waandamanaji 50 waliokuwa wamepiga kambi kusogea karibu na mkahawa maarufu wa kikao hicho cha kilele.Marais 15 walijadilia masuala ya misaada na maendeleo barani Afrika huku mataifa wanachama wa G8 wakishinikizwa kutimiza ahadi zao za misaada.


Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel alisema kuwa viongozi wa mataifa ya Afrika wanataka hatua kuchukuliwa ili kupambana na ongezeko la bei za mafuta na chakula ulimwenguni kwani bara hilo ndilo linaloathirika zaidi.


Marais wa Algeria,Ghana,Nigeria,Senegal,Afrika Kusini na Tanzania wanahudhuria kikao hicho cha Tokayo.Bei za vyakula zimeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kusababisha maandamano katika baadhi ya nchi za Afrika.Bara hilo aidha linatatizwa na ongezeko la bei za mafuta.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aliyehudhuria ufunguzi rasmi wa kikao hicho anawaunga mkono viongozi wa Bara la Afrika na kutoa wito kwa viongozi wa kundi la G8 kutimiza ahadi zao.Bwana Ban Ki Moon aliongeza kuwa atafanya mazungumzo na viongozi wa bara hilo kuhusiana na suala la Zimbabwe vilevile kuchagiza hatua zaidi kuchukuliwa ili kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya anga.


Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa zinasisitiza kauli za kuongeza kiwango cha msaada kwa bara la Afrika.Azma ya hatua hiyo ni kukwamua mamilioni ya wakazi wa bara la Afrika kutoka minyororo ya umasikini.

Miaka minane iliyopita marais pamoja na viongozi wa serikali kutoka kote ulimwenguni waliridhia kutimiza malengo ya milenia ya maendeleo ifikapo mwaka 2015.Baadhi yake yanajumuisha kupunguza umasikini kwa nusu vilevile uhaba wa chakula,elimu ya msingi kwa watoto wote pamoja na kupunguzwa idadi ya vifo vya watoto.


Mwaka jana mataifa wanachama wa G8 walichanga dola bilioni 18.8 ili kuimarisha bara la Afrika na kuahidi kuongeza kiwango hicho hadi dola bilioni 40 kwa mwaka mpaka ifikapo mwaka 2010.Hata hivyo kasi ya kutimiza malengo hayo imepungua na ongezeko la bei za vyakula na mafuta ulimwenguni vinatatiza zaidi mpango huo.

Kwa upande mwingine viongozi wa kundi la G8 wanashinikiza hatua ya kuiwekea Zimbabwe vikwazo zaidi baada ya rais Robert Mugabe kujinyakulia muhula wa sita katika duru ya pili ya uchaguzi batili mwishoni mwa mwezi uliopita.Kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai alisusia duru ya pili ya uchaguzi huo kwa madai ya kukithiri kwa vitendo vya mateso dhidi ya wafuasi wake.


Wakati huohuo Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Jean Ping alikimbizwa hospitalini baada ya kuugua ghafla wakati wa kikao cha kundi la G8.Bwana Ping aliye na umri wa miaka 65 na raia wa Gabon alilamika kuwa hajisikii vizuri wakati wa mkutano huo kwa mujibu wa shirika la habari la Japan la Kyodo.Bwana Ping alitibiwa katika hospitali moja mjini Sapporo ulio karibu na anaripotiwa kuwa hali nzuri.