1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yajadili mizozo, uhamiaji na miradi ya maendeleo

Grace Kabogo
29 Januari 2018

Marais wa nchi za Umoja wa Afrika wamejadili kuhusu kufadhili miradi ya maendeleo ya umoja huo, tatizo la uhamiaji na ufumbuzi wa migogoro kwenye nchi kadhaa na kwamba bila mshikamano maendeleo ni ndoto barani Afrika.

https://p.dw.com/p/2rgXa
Äthiopien Addis Abeba Afrikanische Union Gipfel Guterres
Picha: Palestinian Presidency

Marais wa nchi za Umoja wa Afrika wamejadili kuhusu kufadhili miradi ya maendeleo ya umoja huo, tatizo la uhamiaji na ufumbuzi wa migogoro kwenye nchi kadhaa. Mwenyeketi mpya wa Umoja wa Afrika, Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema bila ya kuwepo mshikamano maendeleo ni ndoto barani Afrika.

Hayo yamezungumzwa wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia. Aidha, mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Rais Alpha Conde wa Guinea, amesema kuwa matatizo ya Afrika lazima yatatuliwe na Waafrika wenyewe.

Conde amekosoa vikali uwajibikaji wa vikosi vya Umoja wa Mataifa barani Afrika na kupendekeza kuweko vikosi vya kikanda vya Waafrika wenyewe chini ya Umoja wa Mataifa

''Tumeona kwamba wanajeshi wa Umoja wa Mataifa hawakuwajibika ipasavyo. Kuna wanajeshi zaidi ya 20,000 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa miaka kadhaa sasa, lakini hakuna matokeo mazuri. Kwa nini tunataka wanajeshi kutoka Bangladesh na Indonesia waje kufa barani Afrika ambako sio kwao? Ili kufa barani Afrika inapaswa awepo mzalendo anayeipenda nchi yake. Leo ni Waafrika wenyewe wanaotakiwa kupigana kwa ajili ya usalama na amani yao wenyewe,'' alisema Rais Conde.

Moussa Faki Mahamat Addis Abeba
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya AU, Moussa Faki MahamatPicha: picture alliance/dpa/L.Baishun

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat ametoa mwito kwa ajili ya ufumbuzi wa mizozo barani Afrika huku akiitolea mfano wa Sudan Kusini ambako ameomba pawepo na vikwazo dhidi ya viongozi wanaokwamisha mchakato wa amani.

Vikwazo kwa wanaokiuka mchakato wa amani

''Nchini Sudan Kusini, kwa nini tusihoji kinachoendelea licha ya pande zote kukiuka mkataba wa amani, huku wakiwaacha raia wanaendelea kutaabika? Wakati umefika tuwawekee vikwazo wale wanaokiuka juhudi za amani. Nchini Burundi, pande zote zinatakiwa kuyapa kipaumbele mazungumzo kwa ajili ya suluhisho la kudumu,'' alisema Faki.

Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika Rais Paul Kagame amesema kwamba maguezi ya mfumo wa Umoja wa Afrika yatafanikiwa kwa kupitia mshikamano wa nchi zote za umoja huo.

Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika, Paul Kagame
Rais wa Rwanda, Paul KagamePicha: Imago/Zumapress/E. Contini

''Hakuna nchi ama kanda inayoweza kujiendeleza yenyewe, tunatakiwa kufanya kazi kwa pamoja. Mageuzi ya kifedha na taasisi za Umoja wa Afrika yatatokana na ukweli kama huo wa mshikamano,'' alisema Rais Kagame.

Mada nyingine itakayojadiliwa leo katika mkutano huo ni pamoja na uhamiaji haramu na vipi Umoja wa Afrika utajifadhili wenyewe.

Wakati huo huo, Rais wa Misri, Abdel Fatah Al-Sissi ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka ujao wa 2019.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW Addis Ababa, Ethiopia
Mhariri: Saumu Yusuf