1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU kujadili matatizo ya utoaji chanjo

Bruce Amani
25 Februari 2021

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo wakati kukiwa na shinikizo la kuharakisha mpango wa utoaji chanjo ya corona barani Ulaya. Kufungwa mipaka na vyeti vya chanjo pia vitajadiliwa

https://p.dw.com/p/3ppkI
EU-China-Gipfel zu Markenschutz
Picha: Reuters/Y. Herman

Mkutano huo wa kilele kwa njia ya video wa viongozi wa jumuiya hiyo yenye nchi 27 wanachama umekuja mwaka mmoja baada ya kuanza mgogoro wa Covid-19, wakati maeneo mengi ya Ulaya yakikumbwa na wimbi la pili la maambukizi -- au la tatu kwa mengine.

Soma pia: Chanjo zaanza kutolewa katika Umoja wa Ulaya

Na sasa mataifa wanachama yanakabiliwa na miripuko zaidi ya aina mpya za virusi hatari kutoka Uingereza na Afrika Kusini. Umoja wa Ulaya umezionya serikali za nchi sita, ikiwemo Ujerumani, kuhusu maamuzi ya upande mmoja ya kuweka vizuizi vya mipakani, wakati nchi zinazowategemea watalii zikiongeza mbinyo wa kuondolewa vikwazo vya usafiri kwa wakati kabla ya kuanza likizo za majira ya joto.

Libanon Beirut | Coronaimpfung
Utoaji chanjo Ulaya ulianza kwa kujikokotaPicha: Marwan Naamani/dpa/picture alliance

Baada ya mwanzo wa kujikokota wa utoaji chanjo kwa Umoja wa Ulaya, -- hasa kwa sababu mpango wa Umoja wa Ulaya ulitegemea chanjo za kampuni kubwa ya dawa ya AstraZenecam ambayo ilitoa kiasi kidogo sana cha chanjo, nchi za Ulaya zinatumai kuwa chanjo hizo zitaongezeka kuanzia Aprili wakati Pfizer/BioNTech na Moderna zimeongeza uzalishaji. Chanjo ya kutolewa kwa wakati mmoja ya kampuni ya Johnson & Johnson huenda pia ikapatikana ifikapo katikati ya Machi.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen lengo lake ni kuwa na asilimia 70 ya watu wazima katika Umoja wa Ulaya kupata chanjo ifikapo katikati ya Septemba mwaka huu.

Tayari mawazo yamegeukia suala la vyeti vya chanjo linaloungwa na nchi kama vile Ugiriki na Uhispania. Maafisa kadhaa wa Umoja wa Ulaya na wanadiplomasia wanaonya kwamba licha ya kuwa wanaunga mkono mpango wa kuwa na rekodi inayoweza kuthibitishwa ya chanjo, ni mapema mno kuzingatia wazo la "paspoti za chanjo" ili kurahisisha usafiri.

Ufaransa na Ujerumani zinapinga, zikihofia kuzuka mgawanyiko wa usafiri kati ya waliopata chanjo ambao ni wachache na walio wengi ambao hawajapata. Hata hivyo, mazungumzo ya mwanzo ya Umoja wa Ulaya tayari yameanza na Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Angani – IATA ambacho kinatarajiwa kuzindua app ya IATA Pass itakayohifadhi data za chanjo.

Nchi zote za Umoja wa Ulaya zina hamu ya kupata mbinu salama ya kufungua safari zake kwa wakati kabla ya msimu wa utali wa Juni hadi Septemba, lakini lazima zishirikiane kuhusu hilo, ili kuepusha kile afisa mmoja wa umoja huo amekiita msimu mpya wa kifo.

AFP