1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU wasitisha majadiliano na Urusi

Hamidou, Oumilkher2 Septemba 2008

Hakuna vikwazo ,isipokua viongozi wanasitisha mazungumzo ili kuishinikiza Urusi iondowe wanajeshi wake toka Georgia

https://p.dw.com/p/F9BX
Vikosi vya Urusi vikiwa njiani kuelekea Ossetia ya kusiniPicha: AP



Viongozi wa Umoja wa Ulaya,wakikutana katika kikao cha dharura jana mjini Brussels wameamua kusitisha mazungumzo ya ushirikiano wa kimkakati pamoja na Urusi na kuelezea pia azma ya kutuma tume ya kusimamia makubaliano ya kuweka chini silaha nchini Georgia.


Katika taarifa yao iliyotangazwa mwishoni mwa mkutano huo wa dharura mjini Brussels,viongozi wa Umoja wa Ulaya wameamua kusitisha mazungumzo ya ushirikiano wa kimkakati hadi Urusi itakapoondowa wanajeshi wake toka Georgia .Wameelezea pia "nia ya kuwajibika zaidi katika eneo hilo.''


Uamuzi wa kutumwa tume ya kusimamia makubaliano ya kuweka chini silaha nchini Georgia unatazamiwa kupitishwa September 15 wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.



Kwa maoni ya mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Javier Solana, tume hiyo mpya itakayoendesha shughuli zake sambamba na ile ya jumuia ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya OSCE,itawekwa hatua baada ya hatua-kwanza lakini katika maeneo yaliyojitenga ya Ossetia ya kusini na Abkhasia nchini Georgia kuchunguza kama mpango wa vifungu sita wa amani uliotiwa saini na marais wa Urusi na Georgia mwezi uliopita, unaheshimiwa na baadae tume hiyo itawekwa pia katika maeneo ya mpakani.


Kwa sasa Umoja wa Ulaya unataka kuona vikosi vya Urusi vinaihama Georgia.Mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya Rais Nicholas Sarkozy wa Ufaransa alizungumza kwa simu na rais Dmitry Medvedev kuhusu suala hilo.Mwishoni mwa mkutano wao wa dharura kansela Angela Merkel alisema "Mazungumzo ya simu ya jana pamoja na rais wa Urusi yalikua ya maana.Tunataraji baadhi ya matatizo,na hasa kuhusu kuondolewa vikosi vya Urusi toka Poti na Senaki yatafumbuliwa."


Rais Nicholas Sarkozy, mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya José Manuel Barroso na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Javier Solana wanatazamiwa kwenda ziarani mijini Moscow na Tblisi Jumatatu ijayo kwa sababu hiyo.


Vyombo vya habari nchini Urusi vinazungumzia juu ya "ushindi wa diplomasia ya Urusi" baada ya Umoja wa ulaya kuamua kutoiwekea vikwazo Moscow.Vyombo vya habari vya Urusi vinahisi kuahirishwa mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kimkakati si tatizo."Wanaogopa wasije wakakosa mafuta ya Urusi" limeandika gazeti linalosomwa na wengi TVOI Den huku IZVESTIA likiandika "Matokeo ya mkutano wa kilele wa Umoja wa ulaya yameonyesha kwamba viongozi wengi wa umoja huo hawataki kuzozana kwa muda mrefu na Urusi."

Nae mwakilishi wa Urusi katika Umoja wa Ulaya Vladimir Tchijov amesema "Kwa kusitisha mazungumzo ya kimkakati pamoja na Moscow,Umoja wa Ulaya unajisumbua wenyewe.''


"Hatutotaharuki.Hatutegemei sana mazungumzo hayo na mkataba huo wa ushirikiano pamoja na Umoja wa ulaya" amesema hayo mwakilishi wa Urusi katika Umoja wa Ulaya.


Mazungumzo ya ushirikiano wa kimkakati yaliyoanza Julai iliyopita na kupangwa kuendelea September 15 mjini Brussels,yanalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi,nishati na kisiasa kati ya umoja wa ulaya na Urusi zilizotiliana saini mkataba kama huo tangu mwaka 1997.