1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G20 wakutana Urusi

5 Septemba 2013

Viongozi wa nchi ishirini zenye uwezo mkubwa kiuchumi wanakutana nchini Urusi kwa mazungumzo yanayonuiwa kuimarisha uchumi wa dunia lakini suala linalotarajiwa kutawala ni mzozo wa Syria

https://p.dw.com/p/19cL0
Picha: DW/Böhme

Viongozi wenye ushawishi mkubwa duniani na walio na misimamo tofauti kuhusu mzozo wa Syria wanakutana leo na kesho Ijumaa mjini St Petersburg nchini Urusi kujadili masuala ya kiuchumi lakini tayari mazingira yameshadhihirisha wazi kuwa ajenda itakayotawala katika mkutano huo ni Syria.

Rais Barrack Obama ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kutaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Syria atakutana na mwenyeji wake Vladimr Putin ambaye amekuwa mshirika mkuu wa Rais Bashar al Assad huku viongozi wengine ambao wamekuwa na usemi mkubwa kuhusu suala hilo akiwemo Rais wa Ufaransa Francois Hollande,Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon,waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na wengineo wakihudhuria mkutano huo wa G20.

Usalama umeimarishwa katika eneo la mkutano huo licha ya kuwa hakutarajiwi maandamano makubwa kama yanayoshuhudiwa katika ile inayoandaliwa katika nchi za magharibi.

Viongozi kadhaa wa nchi wanaohudhuria mkutano wa G20 Urusi
Viongozi kadhaa wa nchi wanaohudhuria mkutano wa G20 UrusiPicha: AFP/Getty Images

Mkutano wa mwaka huu utakuwa wa kwanza kutoshughulikia suala la kiuchumi la dharura tangu nchi hizo ishirini zenye uwezo mkubwa wa kiuchumi kuzingatia sana kuhusu mzozo wa kiuchumi uliokumba nchi nyingi mwaka 2008.

Ukuaji wa uchumi na ajira miongoni mwa ajenda kuu

Badala yake mazungumzo hayo yatajikita katika jinsi ya kufufua uchumi ambao bado unatetereka katika sehemu nyingi duniani na umuhimu wa kuchochea ukuaji na kubuni nafasi zaidi za ajira.Pia miongoni mwa yaliyoko kwenye ajenda ni jinsi ya kuepusha ukwepaji kodi.

Makundi ya wanaharakati yanataka viongozi kuungana kulishughulikia tatizo la ufisadi na makampuni kukwepa ulipaji kodi wakitumai hili likitatuliwa, basi uchumi unaweza kukua na kuimarika .

Nchi ambazo zinainukia kiuchumi ambazo ukuaji wao ulisaidia ukuaji wa uchumi duniani miaka mitano iliyopita zinakabiliwa na matatizo kutokana na kubadilishwa kwa sera za kiuchumi za Marekani ambazo zinafanya mazingira ya kuchochea uchumi kuwa magumu na kusababisha wawekezaji kuanza kuondoka katika nchi zinazostawi.

Licha ya ajenda za mkutano huo kutarajiwa kutuwama kuhusu masuala ya kiuchumi,mzozo wa Syria unatishia kughubika masuala hayo ya kiuchumi na biashara.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Lakhdar Brahimi
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Lakhdar BrahimiPicha: Getty Images

Mjumbe maalum umoja wa Mataifa kuhusu Syria Lakhdar Brahimi anaelekea Urusi kujiunga na viongozi wa G20 ili kunadi haja ya kuandaliwa kwa mkutano wa amani kutatua mzozo wa Syria.

Syria kufunika ajenda rasmi

Misururu ya mikutano miongoni mwa viongozi wa G20 inaashiria kuwa Syria ndiyo inayogonga vichwa vya viongozi hao.Ikulu ya Rais wa Marekani imesema Obama atakutana pembezoni mwa mkutano huo na Rais wa Ufaransa Francois Hollande pamoja na viongozi wa China na Japan.

Ingawa hakujakuwa na taarifa rasmi iwapo kutakuwa na mkutano rasmi kati ya Obama na mwenyeji wake Putin,duru zinaarifu huenda kukawa na mazungumzo fulani kati yao.Obama alifutilia mbali mazungumzo ya ana kwa ana na Putin kutokana na kuzidi kwa uhasama kati yao.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umezidi kuzorota kuhusu mzozo wa Syria na kupewa hifadhi kwa mfichua siri za Marekani Edward Snowden.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/afp/ap

Mhariri: Ssessanga Iddi Ismail