1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Israel na Palestina kukutana.

8 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CmRn

Jerusalem. Viongozi wa Israel na Palestina wanakutana leo Jumanne siku moja kabla ya ziara ya rais wa Marekani George W. Bush kuwasili katika eneo hilo, ili kujaribu kutafuta kupata kupiga hatua kwa mazungumzo ambayo hayajasongambele tangu ulipofanyika mkutano wa amani ya mashariki ya kati uliodhaminiwa na Marekani Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani Stephen Hadley amesema mjini Washington kuwa rais Bush anakwenda katika eneo hilo ikiwa ni nafasi ya kulijadili suala hilo na viongozi wa Israel na Palestina.

Vikao vya majadiliano tangu kufanyika mkutano huo Novemba mwaka jana mjini Annapolis , Maryland, vimechafuliwa na mipango ya Israel ya upanuzi wa ujenzi zaidi wa makaazi, katika maeneo yanayogombaniwa pamoja na mashambulizi ya Wapalestina dhidi ya Israel.

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais wa Palestina Mahmoud Abbas watajadili leo masuala ya utaratibu , ikiwa ni pamoja na wapatanishi gani watapewa jukumu la kujadili masuala mbali mbali ambayo yanagawa pande hizo mbili.

Mazungumzo hayo yatafanyika katika ofisi ya waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert mjini Jerusalem, na viongozi hao wameahidi kufikia makubaliano muhimu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu 2008.