1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakubaliana ujenzi wa miundombinu

30 Novemba 2012

Viongozi wa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki wamekubaliana kujenga miundombinu ya usafiri wa reli na bandari ili kuimarisha uchumi wa eneo hilo.

https://p.dw.com/p/16tUf
Rais Mwai Kibaki wa Kenya
Rais Mwai Kibaki wa KenyaPicha: AP Photo

Kwenye makubaliano hayo, Viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki wameafikiana kwa pamoja kuanzisha mpango wa ujenzi wa miradi ya miundombinu katika kipindi cha miaka kumi ijayo. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa barabara, reli, bandari na uzalishaji kawi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti anayeondoka wa Jumuiya hiyo, Rais Mwai Kibaki, amesema hatua hiyo itasaidia sana eneo hilo.

“Kwa wakati huu mizigo inayosafirishwa kwa reli ni chini ya asilimia tano na hiyo inaweka mzigo mkubwa kwa usafiri wa barabara. Huku kiwango cha mizigo kikitarajiwa kuongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka 15 ijayo, tatizo la usafiri litazidi kuwa kubwa. Kwa hivyo ipi haja kwetu sisi kuwekeza ipasavyo na kupanua mifumo yetu ya reli”.

Viongozi hao wamesema kwamba kuna haja ya ushirikiano kati ya mataifa wanachama wa jumuia ya Afrika mashariki na nchi jirani ili kujenga miundonsingi ya kuunganisha maeneo ya kiuchumi yuanayopakana na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Museveni achukuwa uwenyekiti

Mwenyekiti anayeshika usukani wa Jumuia ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amesema licha ya Jumuiya hiyo kubuni soko la pamoja tangu kuanzishwa kwake, lakini halina miundombinu ya kuridhisha.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: dapd

“Jumuia ya Afrika Mashariki ilibuni soko la watu milioni 140, Jumuia ya Kiuchumi ya COMESA ina soko la watu milioni 300 nayo Jumuia ya Kiushumi ya Kusini mwa Afrika SADC ina soko la watu wapatao milioni 230. Hata hivyo masoko haya hayana miundomsingi na nishati ya kuendesha uzalishaji bidhaa.” Amesema Museveni.

Mkutano wa Viongozi umekuwa kilele cha msururu wa shunguli zilizoanza na kikao cha Baraza la mawaziri kujadili maswala muhimu yakiwemo kuweko mfumo wa pamoja wa forodha na ambi la Sudan Kusini na Somalia kujiunga na Jumuia ya Afrika Mashariki.

Shughuli zilizotangulia ni ufunguzi wa makao makuu ya jumuia na kisha kufunguliwa kwa barabara ya kutoka Arusha, Tanzania kuelekea Arthi River Kenya kupitia Namanga siku ya Jumatano.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa barabara hiyo, Rais Jakaya Kiwete wa Tanzania alisema hayo ni matunda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Ni kutokana na juhudi za pamoja kati ya nchi hizi mbili Kenya na Tanzania ambapo tuliweza kupata fedha kutoka kwa Benki ya Mandeleo barani Afrika na Serikali ya Japan kujenga barabara hii ya Arusha Namanga Athi River tunayoifungua leo,” alisema Kikwete.

Kuhusu ombo la Sudan Kusini kujiunga na Jumuia ya Afrika Mashariki, viongozi wa mataifa wanachama wameliagiza baraza la mawaziri wa jumuia hiyo kuendelea klijadili swala hilo.

Hatima ya Somalia kujiunga na Jumuia bado haijajulikana kwani swala la usalama ndani ya Somalia limekuwa kikwazo kwa nchi hiyo kuwa mwanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki hadi usalama utakapoimarika. Hata hivyo viongozi wa Jumuia wamejitolea kuunga mkono juhudi za kuleta amani nchini Somalia.

Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef