1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Jumuiya ya Ulaya wanakutana leo mjini Brussels.

28 Oktoba 2010

Kuna mpasuko kuhusu uwezekano wa kuufanyia mabadiliko mkataba wa Lisbon.

https://p.dw.com/p/Pqzi
Nembo ya Jumuiya ya Ulaya ambayo ina mataifa 27 wanachama. 16 yanatumia sarafu ya Euro.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo mjini Brussels kuyajadili masuala mazito kuhusu mbinu na mwelekeo utakaofuatwa katika kudhibiti hali ya kifedha na kiuchumi katika umoja huo.

Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman von Rompuy amesema katika muhula uliopita, wanachama wa Umoja huo walifanya maamuzi mazito na wakashinda katika vita vya kuilinda sarafu ya Euro na alitoa mfano wa jinsi Ugiriki ambayo ni mwanachama, ilivyokwamuliwa mwezi Mei ilipokuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa ya madeni. Bw Rompuy aliyasema hayo kabla ya mkutano utakaoanza mjini Brussels na ambao umetabiriwa utakumbwa na malumbano.

Katika ajenda kuu ya mkutano huo wa siku mbili, ni mapendekezo mazito yatakayowasilishwa baada ya miezi kadhaa ya majadiliano yanayonuia kuimarisha udhibiti wa kiuchumi katika Umoja wa Ulaya ambao una kiasi ya raia nusu bilioni. Hata hivyo wachunguzi wanadai kwamba mapendekezo ya dakika za mwisho ya Ujerumani na Ufaransa yanaweza kuvuruga uwezo wa Jumuiya hiyo wa kukabiliana na mzozo wa kifedha.

Nchi hizo mbili zenye usemi katika Umoja wa Ulaya, zinataka mabadiliko yatekelezwe katika mkataba wa Lisbon ambao unauongoza Umoja huo.

Mkataba huo ulikubalika baada ya mazungumzo ya takriban miaka kumi kabla ya kuanza kutekelezwa Disemba mwaka jana. Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na rais wa Ufaransa Nikolas Sarkozy wanautaka mkataba huo wa Lisbon ufanyiwe mabadiliko ili kuwe na hazina ya kudumu ya kuyakwamua mataifa yatakayolemewa kiuchumi na pia kipengee kitakachotoa adhabu kwa nchi wanachama zitakazokuwa na matumizi makubwa, kikiwemo kuondolewa kwa haki zao za kupiga kura.

Martin Schulz, mwanachama wa chama cha SPD hapa Ujerumani, katika bunge la Ulaya amesema kutokana na mgogoro wa fedha,matumizi yanapunguzwa katika kila sekta.

Kodi zimepandishwa katika baadhi ya nchi, muda wa kufanya kazi umerefushwa na pensheni kupunguzwa. Wakati huo huo alisema mabenki na mashirika ya bima yanachuma faida kubwa na kwamba anafikiri mambo hayo yanawaghadhabisha watu.

Matukio hayo yanajiri siku moja tu baada ya waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutoa mwito kwa wanachama wa Umoja wa Ulaya kupitisha bajeti ya chini kabisa kwa kipindi cha mwaka 2011 ili iwe wazi kwamba Umoja huo unadhibiti masuala yake ya kifedha kikamilifu. Msemaji wa Bw Cameron alisema waziri mkuu huyo tayari amezungumza na rais wa Umoja wa Ulaya, Herman von Rompuy, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, rais Sarkozy wa Ufaransa na pia waziri mkuu wa Ubelgiji, Yves Leterme.

Katika mkutano wa Brussels, mada zingine zitakazopewa uzito ni msimamo wa pamoja kabla ya mkutano wa mataifa yalioko katika kundi la G20 na pia kuhusu mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa utakaofanyika mjini Cancun Mexico mwishoni mwa mwaka huu.

Mwandishi: Peter Moss /Reuters/AFP

Mhariri: Aboubakary Liongo