1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Kiarabu wakutana Mauritania

26 Julai 2016

Ni viongozi saba pekee kati ya 22 ndiyo waliofanikiwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu ambao umefanyika nchini Mauritania kwa mara ya kwanza. .

https://p.dw.com/p/1JVve
Baadhi ya viongozi wa Mataifa ya kiarabu waliokutana nchini Mauritania.
Baadhi ya viongozi wa Mataifa ya kiarabu waliokutana nchini Mauritania.Picha: picture-alliance/dpa/Emirates News Agency

Viongozi waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais wa Yemeni Abed Rabbo Mansour Hadi, Rais wa Sudan Omar al-Bashir, kiongozi wa Qatari Emir Tamim Al- Than ambapo waliunga mkono hatua ya Ufaransa ya kuandaa mkutano wa kimataifa wa amani mwishoni mwa mwaka huu kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mgogoro unaoendelea sasa kati ya Israel na Palestina. Israel imekuwa ikipinga hatua hiiyo ikisisitiza juu ya haja ya kuwepo kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati yake na Palestina na pasipo sharti lolote.

Viongozi hao pia walisisitiza mwito wao wa kutaka kuwepo na taifa huru la wapalestina katika ukingo wa magharibi na pia katika ukanda wa Gaza eneo ambalo sehemu kubwa imekuwa ikikaliwa zaidi na Israel tangu mwaka 1967. Agenda ya Misri ya kutaka kupenyeza ushawishi wake katika mkutano huo wa kutaka kuwepo kwa mazungumzo ya amani kuhusiana na mgogoro wa Israel na Palestina safari hii haikupewa uzito mkubwa sana hasa pia kutokana na kukosekana kwenye mkutano huo Rais wa Misri Abdel Fatah el- Sissi.

Akizungumza katika mkutano huo Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz alisema wakati sasa umefika wa kutafuta ufumbuzi utakaowezesha kupatikana kwa taifa huru la Palestina. Aidha viongozi hao wa mataifa ya kiarabu walionekana kukerwa na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa kwa kutumia jina la kiisilamu na kutaka kuwepo kwa mikakati ya mataifa ya kiarabu katika kutafuta suluhisho la suala hilo.

" Kufanyika kwa mkutano huu wa kilele wa Jumuiya ya mataifa ya kiarabu mjini Nouakchott limekuwa ni tukio la kihistoria nafasi ambayo wanachi wa Mauritania wamekuwa wakiisubiri kwa muda mrefu " alisikika akisema Rais huyo wa Mauritania.

Viongozi wengine wenye ushawishi mkubwa ambao hawakushiriki mkutano huo ni pamoja na Mfalme Salman wa Saudi Arabia na mwanae Mohammed bin Salman, Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, viongozi wa mataifa ya Tunisia, Algeria na kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas.

Ahmed Abul Gheit kuiongoza Jumuiya hiyo

Viongozi waliohudhuria mkutano huo walimchagua waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Misri Ahmed Abul Gheit kuiongoza Jumuiya hiyo.

Mkutano wa Jumuiya ya matifa ya kiarabu ukiendelea nchini Mauritania
Mkutano wa Jumuiya mataifa ya kiarabu ukiendelea nchini MauritaniaPicha: picture-alliance/dpa/Emirates News Agency

Abdul Gheit alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Misri kabla ya vuguvugu lililomuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hosn Mubarak.

Mkutano huo nusura uingie dosari baada ya waziri wa Afya wa Lebanon Wael Abu Faour kuzungumza katika televisheni moja nchini humo akisema nchi ambayo iliandaa mkutano huo haikustahili kupata heshima hiyo kutokana na kukosa miundo mbinu ya uhakika na pia mkutano huo kufanyika katika hema akilinganisha na mikutano iliyopita ambayo ilikuwa ikifanyika katika hoteli za nyota tano au katika kumbi za mikutano za kimataifa. Hatua hiyo ilipelekea mwandishi mmoja wa habari maarufu wa Palestina Abdul- Bari Atwan kumkosoa Waziri huyo kutokana na makala aliyoiandika kupitia gazeti la mtandaoni la Rai Al-Youm akisema anashindwa kuelewa jeuri inayoonyeshwa na viongozi wanaodai kuwa ni warabu dhidi ya nchi ya Mauritania kwa vile tu ni taifa maskini kutokana na kukosa mafuta na dhahabu.

Viongozi hao wa mataifa ya kiarabu wamekubaliana mkutano ujao wa kilelele wa Jumuiya hiyo ufanyike nchini Yemen licha ya mgogoro unaoendelea nchini humo.

Walitoa mwito kwa pande mbili zinazozozona katika mgogoro huo wa Yemen kuruhusu njia ya majadiliano kutawala katika mazungumzo ya amani yanayoendelea sasa nchini Kuwait ili kurejesha amani nchini humo.

Mwandishi: Isaac Gamba/ DPAE/ APE/DW

Mhariri: Josephat Charo