1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Muslim Brotherhood wakamatwa Misri

28 Januari 2011

Serikali ya Misri imewakamata watu kadhaa wakiwemo viongozi wanane wa kundi la upinzani la Udugu wa Kiislamu, wakati wananchi wakijiandaa kwa maandamano makubwa baada ya sala ya leo ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/106Ty
Askari wakikabiliana na waandamanaji mjini Cairo
Askari wakikabiliana na waandamanaji mjini CairoPicha: AP

Kukamatwa kwa wapinzani hao kumefanyika usiku wa kuamkia leo (28 Januari 2011), baada ya kundi hilo kuwataka wanachama wake kushiriki katika maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika leo mchana.

Takriban watu 1,000 wamekamatwa tangu kutokea kwa maandamano hayo, ambako waandamanaji wamekuwa wakitoa wito wa kuwepo kwa demokrasia, kumuondoa madarakani Rais Hosni Mubarak, ambaye yuko katika utawala kwa miaka 30 sasa na pia waandamanaji hao wanataka fursa zaidi katika ajira.

Mitandao ya mawasiliano yavurugwa

Ulinzi mkali katika miji kadhaa nchini Misri
Ulinzi mkali katika miji kadhaa nchini MisriPicha: picture alliance / dpa

Ili kudhibiti usambazaji wa habari, katika jitihada za kuzuia kufanikisha maandamano hayo, jana usiku, mawasiliano ya mtandao wa Internet yamevurugwa na pia kuzuia mitandao ya kimataifa ya habari, pamoja na mtandao wa serikali ya nchi hiyo na ule wa ubalozi wa Marekani mjini Cairo. Na pia kuzuia kutuma ujumbe mfupi wa SMS.

Wakati maandamano hayo yakiwa yamepanga kufanyika mchana wa leo habari zinasema majeshi ya ulinzi yameondoka katika mitaa ya mji mkuu wa Misri, Cairo.

Wamisri wamekuwa wakitarajia kuwepo kwa polisi wengi wakati wa maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika baada ya sala ya Ijumaa, lakini badala yake hadi muda mfupi uliopita hakukuonesha dalili za kuwepo kwa polisi wa kiutuliza ghasia hususan katika mitaa muhimu ya mji huo, hususan katika maeneo ambao polisi wamekuwa wakionekana hata katika siku za kawaida.

El Badarei arejea

Mohammed El-Baradei
Mohammed El-BaradeiPicha: AP

Akizungumza jana baada ya kurejea nchini humo, kiongozi wa upinzani nchini Misri, Mohamed El Baradei, ambaye pia mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel na mkuu wa zamani wa Shirika la kimataifa la nguvu za Atomic, alisema amerudi nchini humo kuhakikisha kuwa kila kitu kitashughulikiwa kwa njia ya amani na kutahadharisha matumizi ya nguvu.

''Pindi utawala utatumia nguvu hatua hiyo haitaleta manufaa yoyote, na itasababisha hali mbaya zaidi."

Waandamanaji nchini Misri wamekuwa wakiwa na matumaini ya kuiga uasi kama uliofanywa nchini Tunisia na kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Zine el Abidine Ben Ali, Januari 14, baada ya karibu miaka 23 ya utawala.

Tayari viongozi mbalimbali dunia ni wametoa kauli zao, juu ya hali ya kisiasa nchini Misri, ambao Rais wa Marekani Barack Obama, kwa upande wake amesema ghasia zinazotokea sasa nchini Misri sio jibu katika kupata ufumbuzi wa matatizo yaliyopo.

Tayari serikali ya Misri imesema haitovumilia kuona maandamano zaidi, lakini upinzani umewahimiza watu kushiriki maandamano hayo ya leo.

Mwandishi: Halima Nyanza/DPA/AFPE/APE
Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhani