1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa NATO kuzuru Georgia kama ishara ya kuiunga mkono nchi hiyo

Mohmed Dahman15 Septemba 2008

Mabalozi wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO leo wanazuru Georgia ikiwa ni ishara ya kuiunga mkono nchi hiyo inayotarajia kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo baada ya kushindwa na vikosi vya Urusi.

https://p.dw.com/p/FIEx
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO Generali Jaap de Hoop Scheffer.Picha: AP

Ziara yao hiyo inakwenda sambamba na mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels ambao pia unafanyika leo hii .

Mjini Brussels Ubelgiji mawaziri hao wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wataendelea kuishinikiza Urusi kuondowa vikosi vyake kutoka Georgia kwa kuidhinisha mipango ya kutuma waangalizi 200 wa makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi ujao huko Georgia kama ilivyokubaliwa katika makubaliano hayo kati ya Georgia na Urusi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter - Steinmeir amezungumzia utumaji wa waangalizi hao wa Umoja wa Ulaya huko Georgia kwa kusema kwamba wako tayari kutowa kikosi cha Umoja wa Ulaya na kwa upande wa Ujerumani kujiunga na kutowa mchango wao katika kikosi hicho ili kuleta utulivu.

Kuingilia kati kwa Urusi nchini Georgia kumelaaniwa na jumuiya ya kimataifa na kuzidisha wasi wasi juu ya utulivu kwa eneo kubwa la Caucasis ikiwa kama ni njia ya kupitishia mafuta na gesi kutoka Bahari ya Caspian kuelekea mataifa ya magharibi kwa kupitia Urusi.

Lakini mataifa ya magharibi yamekwepa kuiwekea vikwazo Urusi kwa kiasi fulani kutokana na nyingi ya nchi hizo kutegemea Urusi kwa usambazaji wa nishati.

Serikali ya Georgia inakiona kikao cha kwanza cha Kamisheni ya NATO na Georgia kuwa ahadi mpya kwa mustakabali wake wa kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo lakini kikao hicho huenda tu kikarekebisha tafauti kati ya nchi wanachama wa NATO juu ya busara ya kutanuka zaidi kuingia kwenye majimbo ya zamani ya Urusi.

Urusi imechukizwa na ahadi ya NATO kuzipatia uwanachama nchi jirani za Georgia na Ukraine.Baadhi ya mataifa ya magharibi yakiwemo Ujerumani na Ufaransa yana wasi wasi wa kiuchukiza Urusi juu ya suala hilo.

Waziri wa masuala ya muungano kati ya Georgia na Ulaya Georgy Baramidze amesema mkutano huo unaonyesha kuzidi kuimarika kwa uhusiano kati ya Georgia na NATO na ni ishara nzito pamoja na kukabiliana na uchokozi wa Urusi dhidi ya Georgia.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO Generali De Hoop Scheffer ataongoza ujumbe wa NATO mjini Tblisi mji mkuu wa Georgia.

Amesema haiwezekani mtu kusema huko Moscow tunaheshimu mipaka ya Georgia na halafu wakati huo huo wanasema tunabakia na wanajeshi 6,000 au 7,000 huko Abkhazia.Mambo hayo hayawezi kwenda pamoja.Sifahamu na pia sifikiri kwamba Umoja wa Ulaya utalikubali hilo.

Katika mji mkuu wa Abkkazia Sukhumi waziri wa mambo ya nje wa Urusi Segei Lavrov amemshutumu Generali huyo wa NATO kwa kutowa taarifa zisizofaa na zisizowajibika kuhusiana na mzozo wa Georgia.

Mkutano wa NATO unakwenda sambamba na safari ya Lavrov huko Ossetia Kusini na Abkhazia majimbo mawili yaliojitenga ya Georgia ambayo kwayo Urusi kwa kupingana na mataifa ya magharibi imeyatambuwa kuwa mataifa huru.

Vikosi vya Urusi vilijipenyeza ndani kabisa mwa Georgia hapo mwezi wa Augusti baada ya kuzima shambulio la Rais Mikheil Saakashvili wa Georgia kulichukuwa tena jimbo lililojitenga la Ossetia Kusini.