1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa SADC kukutana

16 Agosti 2015

Viongozi wa mataifa 15 ya kusini mwa Afrika watakusanyika kwa ajili ya mkutano wa kila mwaka kesho Jumatatu (17.08.2015) wakati eneo hilo linakumbwa na matatizo makubwa ya upungufu wa chakula.

https://p.dw.com/p/1GGBD
Deutschland SADC-Delegation besucht Sauerland
Viongozi wa SADC walipotembelea UjerumaniPicha: DW/S. Duckstein

Mkutano huo unakuja wakati eneo hilo linakumbwa na matatizo makubwa ya upungufu wa chakula ambao umesababisha idadi kubwa ya watu wakihitaji msaada.

Katika mchanganyiko wa mvua zinazonyesha kwa ghafla, joto kupita kiasi na mafuriko, vimeharibu mashamba na kupunguza kiasi kikubwa cha mazao ya msimu huu.

Simbabwe SADC Gipfel in Harare - Robert Mugabe
Rais wa Zimbabwe Robert MugabePicha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Watu wanaokadiriwa kufikia milioni 27.4 kutoka idadi jumla ya wakaazi milioni 292 wa eneo hilo ama karibu mmoja kati ya watu kumi watategemea msaada wa chakula ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Mavuno yapungua

Mavuno ya mahindi yamepungua kwa asilimia hadi 90 katika baadhi ya nchi za mataifa hayo 15 wanachama wa jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC, ripoti ya mwezi Juni iliyotolewa na kundi hilo imesema.

"Kutokana na matatizo hayo yanayolikabili eneo hilo, idadi ya watu ambao hawana usalama wa chakula imeongezeka kwa asilimia 13 hadi milioni 27.4 mwaka huu ikilinganishwa na watu milioni 24.3 mwaka uliopita," ripoti hiyo imesema.

Sambia Entwicklungsgemeinschaft Südliches Afrika Treffen
Viongozi wa SADC katika mkutanoPicha: AP

Lakini viongozi wanaokutana nchini Botswana kuanzia kesho Jumatatu hawatarajiwi kutoa wito wa kimkoa kuomba msaada.

"Badala yake, nchi binafsi zitafanya hivyo," amesema margaret Nyirenda, mkurugenzi wa idara ya chakula, kilimo na mali asili wa SADC.

Malawi, Zimbabwe, Namibia na Botswana ni miongoni mwa nchi zilizoathirika mno. Msemaji wa shirika la mpango wa chakula wa dunia David Orr ameliambia shirika la habari la AFP Zimbabwe na Malawi zinakabiliwa na mzozo mkubwa wa usalama wa chakula katika miongo kadhaa.

Zimbabwe imeathirika pakubwa na upungufu wa chakula

Zimbabwe ikiwa na upungufu wa asilimia 49, itahitaji kuagiza kutoka nje tani 700,000 za nafaka ya mahindi kuweza kuwalisha wakaazi wanaofikia milioni 1.5.

Makamu wa Rais nchini humo Ermmerson Munangagwa tayari ametoa wito wa kupatiwa fedha kutoka katika mashirika ya maendeleo pamoja na sekta binafsi kuhakikisha kwamba watu wenye matatizo ya chakula hawafikii kukabiliwa na njaa na kufa.

Dürre in Südafrika 2011
Ukame wa muda mrefu huadhiri kilimoPicha: Getty Images/AFP/A. Abdulle

Nchini Malawi mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo mapema mwaka huu yameharibu mashamba na kusababisha vifo vya watu 176. Kimsingi ni nchi ya tatu kwa uzalishaji mahindi katika eneo hilo lakini mwaka huu imelazimika kuagiza mahindi kutoka nchi jirani ya Zambia.

Kwa mujibu wa makadirio rasmi, hadi watu milioni 2.8 nchini Malawi watahitaji chakula cha msaada ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wakati upungufu wa chakula utakapokuwa mkubwa.

Eneo la kilimo Botswana limeathirika na ukame

Upungufu mkubwa wa mvua pamoja na joto kali nchini Botswana, wakati huu, vimesababisha upungufu wa asilimia 70 katika maeneo yanayolimwana asilimia 90 ya upungufu wa mazao.

Afrika Dürre Landschaft Hunger
Eneo la kilimo limeathirika kutokana na ukame wa muda mrefuPicha: AP

Nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini ya almasi Imetenga dola milioni 44 katika mfuko wa dharura kupambana na kile serikali inachosema ni ukame mbaya kabisa kuikumba nchi hiyo katika miaka 30.

Na wakati nchi inayozalisha kwa wingi nafaka Afrika kusini ikirekodi upungufu wa asilimia 31 katika uzalishaji mwaka huu, hofu imetanda ya athari za mtikisiko nchini Swaziland, Botswana na Lesotho.

Mavuno ya sasa ya mahindi nchini Afrika kusini , ni"mavuno ya chini kabisa tangu mwaka 2007," idara ya kilimo nchini humo imeliambia shirika la habari la AFP, na kuongeza kwamba nchi hiyo itahitaji kuagiza kutoka nje kiasi ya tani 600,000 za mahindi kuweza kuziba upungufu na kutimiza jukumu lake la kimkataba la kuuza nje.

World Food Programme Nahrungsmittellieferung Flugzeug
Shirika la mpango wa chakula duniani linapanga kutoa msaada kwa mataifa ya SADCPicha: AP

Vipindi virefu vya ukame katika baadhi ya sehemu za eneo hilo vimepunguza eneo la malisho kwa wanyama na huenda hali hiyo ikasababisha kupanda kwa bei ya nyama, maziwa, kuku na mayai.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afp

Mhariri: Caro Robi