1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya kuimarisha shinikizo dhidi ya Putin

Abdu Said Mtullya20 Machi 2014

Mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya unaanza leo mjini Brussels ambako viongozi hao wanatarajiwa kuliimarisha shinikizo dhidi ya Urusi.

https://p.dw.com/p/1BT7W
Rais wa Halmashuri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel BarrosoPicha: John Thys/AFP/Getty Images

Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikuwa wayajadili masuala ya ustawi wa uchumi ,nishati na mabadiliko ya sera ya tabia nchi.

Lakini badala yake suala la Ukraine ndilo litakalopewa kipa umbele kutokana na kuzidi kwa mvutano baina ya nchi za Umoja wa Ulaya na Urusi baada ya Rais Putin kuitia saini rasimu juu ya kuliingiza jimbo la Krimea katika shirikisho la Urusi.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Hermann Van Rompuy na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja huo Jose Manuel Barroso wamethibitisha kwamba suala la Ukraine ndilo litakalokuwa la kipaumbele kwenye mkutano.Naye Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Cathrine Ashton amesisitiza kwamba suala la Ukraine litakuwa mbele katika ajenda.

Mazungumzo na Urusi hayatafanyika

Umoja wa Ulaya umeshayafuta mazungumzo ya kisiasa na Urusi na wiki hii ulitangaza vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Hata hivyo serikali za nchi za Umoja wa Ulaya bado hazijaufikia msimamo wa pamoja juu ya suala hilo.Baadhi ya nchi hususan zile zenye uhusiano mkubwa wa kibiashara na Urusi zinahofia kuchukua hatua kali zaidi zinazoweza kuzifunga njia zote za mazungumzo na Urusi.

Waziri wa mambo ya nje wa Austria Sebastian Kurz ametahadharisha juu ya kufanya pupa katika kuchukua hatua za kiuchumi dhidi ya Urusi wakati Bulgaria inayotegemea gesi kutoka Urusi imesema inapinga kuchukuliwa hatua za haraka za kuiwekea Urusi vikwazo vikali. Lakini Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier amesema vikwazo dhidi ya Urusi haviwezi kukwepeka ikiwa Urusi itaendelea kujitandaza zaidi.

Katibu Mkuu kufanya ziara Urusi na Ukraine

Wakati huo huo Katibu Muuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anatarajiwa kuwasili Moscow kwa ajili ya mazungumzo na Rais Wladimir Putin na viongozi wengine wa Urusi juu ya mgogoro wa Ukraine. Katibu Mkuu Ban, pia atafanya ziara Ukraine katika juhudi za kutafuta suluhisho la kidiplomasia.

Mabalozi watoleana kauli kali

Kwenye Umoja Mataifa mabalozi wa Urusi na Marekani walitoleana kauli kali kuhusiana na mgogoro wa Ukraine. Balozi wa Marekani Samantha Power ameiita Urusi kuwa ni mwivi kwa sababu ya matukio ya jimbo la Krimea. Na Balozi wa Urusi, amesema kuwa kauli za kashfa zilizotolewa na Balozi wa Marekani dhidi ya nchi yake zitauhatarisha ushirikiano baina ya nchi zao.

Nchini Ukraine kwenyewe serikali ya muda imearifu kwamba inaandaa mipango ya kuwaondoa wanajeshi wake kutoka jimbo la Krimea .

Mwandishi:Bernd Riegert.

Tafsiri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman