1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wakutana kuzungumzia 'mfumo wa dijitali'

Oumilkheir Hamidou
29 Septemba 2017

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Tallinn, Estonia, kuzungumzia "mfumo wa dijitali" licha ya kugubikwa na mjadala uliotokana na mapendekezo ya rais wa Ufaransa kuhusu mustakbali wa Umoja huo.

https://p.dw.com/p/2kxPV
Estland Tallinn EU-Gipfel Digital Summit 28.09.2017
Picha: Reuters/V. Mayo

Majadiliano yatakayoanza jioni ya leo (Septemba 29) yanatarajiwa kugubikwa na pendekezo la Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa la jinsi ya kutozwa ushuru makampuni makubwa makubwa ya kidijitali mfano wa Apple au Google, yanayotuhumiwa kutolipa ipasavyo kodi ya mapato.

Ufaransa inapendelea kuona makampuni makubwa makubwa mfano wa Google au Apple yakitozwa ushuru unaostahiki badala ya mtindo unaotumika hivi sasa wa kutozwa katika nchi moja tu ya Umoja wa Ulaya, mfano wa Ireland au Luxemburg, kodi ya mapato kwa shughuli za kibiashara walizofanya katika nchi zote za Umoja wa Ulaya.

Mada hiyo italeta malumbano katika mkutano huo wa kilele, ingawa haijaorodheshwa katika ajenda ya mazungumzo.

Lakini mbali na dijitali, suala la mustakbali wa Umoja wa Ulaya linategemewa kuhodhi mazungumzo mnamo wakati ambapo Umoja wa Ulaya unatafakari njia ya kufuata baada ya jinamizi la Brexit.

Kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Getty Images/V. Kalnina

Umoja wa Ulaya unaokwenda kwa kasi tofauti

Mada hiiyo ililetwa mazungumzoni katika karamu ya chakula cha usiku jana ambapo viongozi wa Umoja wa Ulaya walizungumzia hotuba ya Macron aliyoitoa katika Chuo Kikuu cha Sorbonne mjini Paris Jumanne iliyopita, akiunga mkono fikra ya kuwepo kwa "Umoja wa ulaya wa kasi za aina tofauti" utakaoendelea kuwa chini ya usukani madhubuti wa Ufaransa na Ujerumani.

"Mimi ninaona kwamba katika hotuba yake hiyo, rais wa Ufaransa ameweka msingi imara wa kuendelezwa ushirikiano kati ya Ujerumani na Ufaransa," alisema Kansela Angela Merkel wa Ujerumani jana usiku na kuongeza ufafanuzi zaidi unahitajika na kwamba nchi hizo mbili zinakubaliana kuwa Umoja wa Ulaya unahitaji kufanyiwa marekebisho.

Viongozi hao wa Ujerumani na Ufaransa walizungumza ana kwa ana kwa muda wa nusu saa jana usiku, bila ya kuyajadili kwa kina mapendekezo ya rais wa Ufaransa, hasa kuhusu kanda ya Euro.

Mwishoni mwa karamu ya chakula cha usiku, viongozi wa Umoja wa Ulaya walielezea azma yao thabiti ya "kuuendeleza umoja" ndani ya Umoja wa Ulaya.

May anashiriki mkutano wa Tallinn

Mwenyekiti wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, atashauriana na viongozi wenzake wiki mbili kutoka sasa kuhusiana na mapendeko ya rais wa Ufaransa kuhusu sera ya pamoja ya uhamiaji.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May na mwenyekiti wa baraza la Ulaya Donald
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May na mwenyekiti wa baraza la Ulaya Donald TuskPicha: Reuters/J. Brady

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, pia alialikwa katika karamu hiyo ya chakula cha usiku.

Uingereza, inayojiandaa kuachana na Umoja wa Ulaya, haikuwa ikialikwa katika mikutano ya hivi karibuni inayozungumzia mustakbali wa Umoja huo.

Leo asubuhi, May alikutana na Rais Macron katika kituo cha Jumuiya ya Kujihami ya NATO mjini Tapa, walikowekwa wanajeshi wa Uingereza na Ufaransa.

Baadaye walitazamiwa kuelekea Tallinn kuhudhuria mkutano wa kilele kuhusu digitali.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu