1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wasema makubaliano ya Brexit hayabadiliki

Sylvia Mwehozi
30 Januari 2019

Maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya wanaohusika na Brexit wamesisitiza kuwa makubaliano ya talaka ya umoja huo na Uingereza hayawezi kujadiliwa upya wakati Theresa May akijiandaa kutafuta maridhiano mapya.

https://p.dw.com/p/3CSZc
Britisches Parlament verhandelt Brexit
Picha: picture-alliance

Uingereza imepangiwa kujiondoa rasmi Umoja wa Ulaya machi 29 mwaka huu, ikiwa nchi ya kwanza kufanya hivyo tangu kuundwa kwa Umoja huo, lakini makubaliano yanayoongoza kujiondoa kwake bado yamekwama kwenye bunge la mjini London, zaidi kwa sababu ya hatua zinazohusiana na suala la mpaka wa Ireland.

Hakikisho hilo linalenga kuibakiza Uingerezaa kwenye umoja wa forodha wa Umoja wa Ulaya ili kuondoa haja ya ukaguzi mipakani baina ya Ireland ya Kaskazini na Jamhuri ya Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya, baada ya Uingereza kujiondoa. Eneo hilo la mpaka wakati mmoja lilikuwa eneo la mapambano katika miongo kadhaa ya mizozo iliyogharimu maisha ya watu wengi.

Wabunge wa Uingereza wanahofu kwamba mpango huo utalifunga taifa hilo ndani ya kanuni za muungano wa Ulaya, na limeyakataa makubaliano ya Brexit ambayo May aliyawasilisha mwezi Novemba na Umoja wa Ulaya. Hapo jana May alipata uungwaji mkono kutoka bungeni wa kufungua tena majadiliano juu ya makubaliano ya kujiondoa , lakini viongozi wa Ulaya wamesisitiza kwamba makubaliano hayo hayawezi kubadilishwa.

Großbritannien Parlament Brexit Abstimmung
Bunge la Uingereza likimsikiliza Waziri Mkuu Theresa MayPicha: picture-alliance/empics

Mkuu wa bunge la Umoja huo Antonio Tajani amesema leo kwamba nchi wanachama 27 zinazosalia kwenye umoja wa Ulaya baada ya Uingereza kujiondoa bado zina mshikamano juu ya suala hilo na hazitajadiliana makubaliano mengine na Uingereza. Amesema ni vigumu kufikiria wanaweza kujadiliana tena makubaliano mengine na Uingereza wakati yalishapitishwa na nchi wanachama wa Umoja huo. Mwakilishi mkuu wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Brexit Michel Barnier amewaeleza waandishi wa habari kuwa.

"Suala muhimu ninalotaka kusisitiza ni kuthibitishwa kwamba taasisi za Umoja wa Ulaya zinasalia kuwa na mshikamano na bado tunasimamia makubaliano yaliyofikiwa na Uingereza".

Naye waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema umoja huo hautaitenga Ireland. "Msimamo wetu uko wazi, makubaliano ya kujiondoa ni bora na suluhisho pekee la kuondoka", alisema Maas. Ameongeza kwamba bado haijawa wazi ni mambo gani ambayo serikali ya Uingereza imeyafanyia marekebisho.

Waziri mkuu Theresa May alitarajiwa kukutana na kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Jeremy Corbyn, ndani ya bunge kwa mujibu wa chanzo kimoja, siku moja baada ya wabunge kumkubalia waziri huyo mkuu afanye majadiliano mapya na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/reuters/ap/afp

Mhariri: Gakuba, Daniel