1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakubaliana mjini Lisbone

Oummilkheir19 Oktoba 2007

Waraka mpya unaochukua nafasi ya katiba inayopingwa,umekubaliwa na viongozi wa umoja wa ulaya

https://p.dw.com/p/C7h0
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Ureno Joose Socrates,mwenyekiti wa zamu wa umoja wa ulaya
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Ureno Joose Socrates,mwenyekiti wa zamu wa umoja wa ulayaPicha: AP

Viongozi wa umoja wa ulaya wanamaliza mkutano wao wa kilele hii leo mjini Lisbonne,baada ya kufikia makubaliano kuhusu mkataba mpya utakaoshika nafasi ya katiba iliyokataliwa.Mkataba huo utabidi hivi sasa uidhinishwe na nchi zote 27 wanachama.

“Ulaya imesawazisha mzozo wa katiba na iko tayari kukabiliana na changamoto zijazo” amesema hayo waziri mkuu wa Ureno José Socrates,mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya,kabla ya kunyanyua bilauri ya Champagne pamoja na viongozi wenzake wa umoja wa ulaya kusherehekea ufanisi huo.

“Tumefanikiwa:tumekubaliana juu ya uamuzi muhimu wa kisiasa” amesema kwa upande wake kansela Angela Merkel wa Ujerumani na kuongeza,tunanukuu:

“Kimsingi hakujakua na yeyote aliyekua na fikra ya kuufuja mkataba huu,kila mmoja alipania kuona makubaliano yanafikiwa.Kwa wakati wote ambapo tutakua na imani kama hiyo,basi Ulaya itafanikiwa.”

Waraka wenye zaidi ya kurasa 250 umeidhinishwa usiku wa jana kuamkia leo,baada ya madai ya Poland na Italy kuhusu utaratibu wa kupiga kura na idadi ya wabunge kukubaliwa.

Poland imepatiwa kifungu cha Ioaninna,kinachoipa usemi mkubwa kisheria kuliko hapo awali.Kifungu hicho kinaziruhusu nchi ambazo hazina idadi kubwa ya wakaazi,zizuwie kwa muda uamuzi uliopitishwa na umoja wa Ulaya.

Italy nayo imepatiwa mbunge mmoja zaidi,idadi ya wabunge wa Ulaya itakapopunguzwa toka 785 na kusalia 750.Kwa namna hiyo idadi ya wabunge wa Italy italingana na ile ya Uengereza.

Waraka huo utabidi kwanza uidhinishwe na mataifa yote 27 ya umoja wa ulaya kabla ya kuanza kufanya kazi.Utaratibu huo tete unaweza kuendelea hadi mwisho wa mwaka ujao.

Viongozi wa umoja wa ulaya wanataraji waraka mpya unaoshika nafasi ya katiba iliyokataliwa utaakufanya kazi mapema mwaka 2009 au kabla ya uchaguzi wa bunge la ulaya ,msimamu wa kiangazi wa mwaka huo huo wa 2009.Waraka huo mpya utatiwa saini mkutanio wa kilele wa Umoja wa ulaya utakapoitishwa December 13 ijayo mjini Lisbone.

Waraka huo umeratibiwa kwa namna ambayo hautahitaji kuidhinishwa kwa kura ya maoni ya wananchi.Waraka huo una vifungu vingi vya katiba ya zamani iliyokataliwa kwa kura ya maoni ya wafaransa na waholanzi.Isipokua neno katiba limeepukwa safarui hii pamoja na vifungu vyote vile vinavyoweza kuonyesha Umoja wa ulaya unageuka dola lenye nguvu:vifungu hivyo ni pamoja na vile vinavyozungumzia wimbo wa taifa na bendera ya Umoja wa ulaya pia.

Irland ndio nchi peke ya umoja wa ulaya itakayolazimika kuitisha kura ya maoni.Uengereza wapinzani wa Umoja wa ulaya wanasdai kura ya maoni iitishwe pia.Lakini waziri mkuu Gordon ameshasema hatoitisha kura hiyo ya maoni.

Hii leo viongozi wa umoja wa ulaya watapitisha siku ya mwisho ya mkutano wao kwa kuzungumzia masuala ya kiuchumi,pamoja pia na kile kijulikanacho kama “mkakati wa Lisbone.”Mkakati huo uliobuniwa mwaka 2000 umelengwa kuugeuza Umoja wa ulaya uwe dola kuu la kiuchumi ulimwenguni hadi ifikapo mwaka 2010.