1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakutana Brussels

10 Desemba 2009

Viongozi wa nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kwa matumaini ya kupata makubaliano kuhusu mpango utakaogharimu mabilioni ya Euro.

https://p.dw.com/p/Kyrn
German Foreign MInister Guido Westerwelle answers questions to media during a press conference at the Cernin's Palace in Prague, Czech Republic on Wednesday, Dec. 2, 2009. (AP Photo/Petr David Josek)
Guido Westerwelle, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani.Picha: AP

Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wao wa siku mbili mjini Brussels vile vile wanataka kuafikiana na kuwa na mkakati mmoja katika majadiliano ya mjini Copenhagen. Lengo ni kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Lakini nchi nyingi zikisitasita kuahidi misaada ya fedha wakati wa hali hii ngumu ya kiuchumi hivi, nchi tajiri za Ulaya ya Magharibi, zitatazamiwa kutoa sehemu kubwa ya msaada wa Euro bilioni sita zitakazohitajiwa katika miaka mitatu ijayo kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Hata hivyo viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels hawatazamiwi kutoa maelezo marefu kuhusu yale yatakayokubaliwa. Na kuna sababu nzuri ya kutofanya hivyo kama anavyoeleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle:

"Nikitaja kiwango fulani cha fedha, basi msimamo wa Umoja wa Ulaya utadhoofishwa katika mkutano wa Copenhagen. Kwa hivyo, hatutotoa hundi iliyowazi ili wengine waweze kukwepa wajibu wao."

Vile vile amesema kuwa Ulaya inataka kuongoza katika ulinzi wa mazingira, lakini haiwezi kuzuia madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa peke yake. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana hii leo na kesho Ijumaa mjini Brussels, wameshasema kuwa wapo tayari kupunguza utoaji wa moshi viwandani kwa asilimia 30 katika kipindi cha miaka kumi ijayo, lakini mwito wa kutoa fedha ni suala jingine.

Bundeskanzlerin Angela Merkel spricht am Donnerstag, 18. Dez. 2008, in Berlin zu Journalisten. Nach dem Messerattentat auf den Passauer Polizeichef Alois Mannichl hat Bundeskanzlerin Angela Merkel ein entschiedenes Handeln der Politik gegen den Rechtsextremismus gefordert. (AP Photo/Michael Sohn) --- German Chancellor Angela Merkel adresses the media after a meeting of the German state governors in Berlin, Germany, Thursday, Dec. 18, 2008. (AP Photo/Michael Sohn)
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.Picha: AP

Kwa maoni ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kinachohitajiwa hivi sasa ni kupatikana makubaliano ya kimsingi yenye mfumo wa kisiasa, utakaoweza kushughulikiwa katika miaka ijayo. Amesema, lengo ni kupata mkataba wa kimataifa unaobidi kutekelezwa ili kuzuia ongezeko la joto kupindukia sentigredi 2 za Celsius.

Kimsingi nchi za Umoja wa Ulaya zipo tayari kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa hadi asilimia 30 badala ya asilimia 20 kama ilivyokubaliwa hapo awali, lakini nchi zingine katika mkutano wa Copenhagen pia ziwe tayari kuchukua hatua kama hiyo. Viongozi wa Umoja wa Ulaya mkutanoni mjini Brussels vile vile watajadili njia za kujitoa kutoka msukosuko wa kiuchumi na kifedha. Miongoni mwa hatua zinazozingatiwa ni kuwepo usimamizi mkali zaidi wa taasisi za fedha. Mkutano wa leo hii mjini Brussels ni mkutano wa kilele wa kwanza kupata kufanywa tangu Mkataba wa Lisbon kuanza kufanya kazi mwanzoni mwa mwezi huu.

Mwandishi:Henn,S/ZPR/P.Martin/AFPE

Mhariri: M.Abdul-Rahman