1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wampongeza Trump licha ya kushtushwa na ushindi

Caro Robi
9 Novemba 2016

Viongozi kutoka kila pembe  ya dunia wameshangazwa na ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa Marekani. Mitizamo na kauli za viongozi wa dunia zinaashiria mashaka, wasiwasi na matarajio yao ya utawala wa Trump.

https://p.dw.com/p/2SOgV
US-Präsidentschaftswahl 2016 - Sieg & Rede Donald Trump
Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Naibu wa Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel amesema Trump ni mwanzilishi wa vuguvugu jipya la kiimla na mfumo dume duniani na kusema ushindi wa Trump ni onyo pia kwa Ujerumani na Ulaya kuwa sharti zibadilike ili kukabiliana na vuguvugu hilo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema ushindi wa Trump sio walioutaka Wajerumani wengi lakini hawana budi kuukubali licha ya kuwa sera za kigeni za Marekani hazitaweza tena kutabirika.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen ameutaja ushindi huo kama mshtuko mkubwa huku waziri wa sheria wa Ujerumani Haiko Maas akisema ulimwengu hautafikia ukingoni lakini mambo yatakuwa ya viroja baada ya ushindi wa Trump.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Marc Ayrault ameahidi kufanya kazi na Trump lakini amesema haiba ya rais huyo mteule inaibua masuali na kukiri kuwa hana hakika utawala wa Trump utamaanisha nini kwa sera muhimu za kigeni, mabadiliko ya hali ya hewa na makubaliano kati ya nchi za magharibi na Iran kuhusu mpango wake wa kinyuklia.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amempongeza Trump na kusema anatumai watakuwa na mazungumzo ya tija kati ya nchi yake na Marekani na kuutoa uhusiano kati ya nchi hizo mbili kutoka kwa mzozo. Wakati wa kampeini Trump alisema anapendezwa mno na utawala wa Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema umoja huo utaendelea kufanya kazi na Marekani na kuongeza uhusiano wao ni mkubwa zaidi ya mabadiliko yoyote ya kisiasa.

US-Präsidentschaftswahl 2016 - Sieg & Rede Donald Trump
Rais mteule wa Marekani Donald Trump na familia yakePicha: Getty Images/M. Wilson

Rais wa bunge la Umoja wa Ulaya Martin Schulz amesema uhusiano kati ya umoja huo na Marekani utakuwa mgumu chini ya utawala wa Trump na kuulinganisha uchaguzi wa Marekani na kura ya maoni ya kujiondoa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amempongeza Rais huyo mteule wa Marekani na kusema ana hamu ya kufanya kazi naye ili kuimarisha uhusiano kati ya nchi zao utakaojikita katika heshima, demokrasia, mitizamo ya pamoja na kuheshimu sheria.

Uturuki kwa upande wake imesema ushindi wa Trump ni fursa ya kuimarisha mahusiano na ukurasa mpya utafunguliwa kuhusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili iwapo Marekani itamrejesha nyumbani Sheikh Fethulah Gulen anayetuhumiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi ya serikali.

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amempongeza Trump na kuzitaja nchi zao kuwa washirika wasiotikisika. Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahamud Abbas amemtaka Trump kushirikiana naye katika kuanzisha taifa la Palestina kupitia suluhisho la mataifa mawili kati ya Israel na Palestina.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihamii ya NATO Jens Stoltenberg amempongeza pia Trump na kusema yuko tayari kufanya kazi naye. Wakati huo huo, vyama vya kisiasa vya mrengo wa kulia vya Australia na Ufaransa vimesherehekea ushindi wa Trump na kuutaja ushindi kwa raia wa kawaida.

Brüssel  Jens Stoltenberg
Katibu mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Reuters/F.Lenoir

Kiongozi wa chama cha Ufaransa kinachowapinga wahamiaji cha National Front Marie Le Pen amempongeza Trump na kusema katika ukurasa wake wa Twitter kuwa watu wa Marekani wako huru. Naibu wake Florian Philippot amesema leo ni Marekani kesho ni Ufaransa. Kiongozi wa chama cha UKIP nchini Uingereza Nigel Farage pia amempongeza Trump.

Beatrix von Storch naibu wa kiongozi wa chama kinachowapinga wahamiaji Ujerumani cha Alternative fur Deutchland AfD amesema ushindi wa Trump ni ishara kuwa raia wa nchi za magharibi wanataka mabadiliko bayana kuhusu sera.

Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban amempongeza rais huyo mteule wa Marekani na kusema ni habari njema zinazoashiria demokrasia bado ipo. Kiongozi mwingine aliyempongeza Trump ni Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi aliyesema anatumai kutakuwa na ukurasa mpya wa uhusiano.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp/ap

Mhariri:Yusuf Saumu