1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi watuma pole kufuatia kifo cha Mugabe

John Juma
6 Septemba 2019

Viongozi mbalimbali wa Afrika na ulimwenguni wanaendelea kutuma risala za rambirambi kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 95 akiwa Singapore akipata matibabu.

https://p.dw.com/p/3P9zZ
Simbabwe Afrika Robert Mugabe
Picha: Reuters/M. Hutschings

Salamu za rambirambi kutoka sehemu mbalimbali duniani zinaendelea kumiminika Zimbabwe, kufuatia kifo cha mwasisi wa utawala wa walio wengi katika taifa hilo la kusini mwa Afrika, Robert Mugabe, ambaye ameaga dunia akiwa matibabuni nchini Singapore. 

Robert Mugabe ambaye aliiongoza nchi yake katika vita vya ukombozi hadi ilipopata uhuru mwaka 1980, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 95, miaka miwili baada ya jeshi kumuondoa madarakani na kukomesha utawala wake wa mkono wa chuma uliodumu kwa takriban miongo minne.

Kufuatia kifo chake, salamu za rambirambi zinazidi kumiminika. Mrithi wake, Rais Emmerson Mnangagwa, amesema kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba Mugabe alikuwa ishara ya ukombozi na mpiganaji wa Afrika aliyejitolea kwa manufaa ya watu wake. Ameongeza kuwa mchango wake katika historia ya bara la Afrika kamwe haiwezi kusahaulika.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema nchi yake inajiunga na Zimbabwe katika kuomboleza kifo cha mpiganiaji ukombozi na mwanaharakati huyo wa umajumui wa Kiafrika dhidi ya ukoloni.

Robert Mugabe aliongoza kwa miaka 37. Utawala wake wa mkono wa chuma ulimalizika mwaka 2017 baada ya jeshi kumshinikiza kung'atuka madarakani.
Robert Mugabe aliongoza kwa miaka 37. Utawala wake wa mkono wa chuma ulimalizika mwaka 2017 baada ya jeshi kumshinikiza kung'atuka madarakani.Picha: picture-alliance/dpa/R. Cooper

Ramaphosa ameongeza kuwa chini ya uongozi wa Mugabe, Zimbabwe iliendelea kuimarisha mapambano ya kishujaa dhidi ya ukoloni hali iliyochochea vita dhidi ya utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini.

Kutoka Beijing, China ambayo ilikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa Mugabe imesema kupitia wizara yake ya mambo ya nchi za nje, kuwa Mugabe alikuwa kiongozi bora wa harakati za ukombozi wa kitaifa na mwanasiasa.

Msemaji wa wizara hiyo, Geng Shuang, amewaambia waandishi wa habari kuwa Mugabe alitetea kabisa uhuru wa ya nchi yake, alipinga uingiliaji wa kigeni na alihimiza urafiki na ushirikiano wa China na Zimbabwe: "Tunatoa pole zetu nyingi kufuatia kifo chake. Pia tunatoa pole zetu kwa serikali ya Zimbabwe na raia wake na kwa familia ya Bwana Mugabe." Amesema Shuang.

Robert Zimbabwe alikuwa mpiganaji wa ukombozi aliyeiongoza nchi yake kupata uhuru mwaka 1980.
Robert Zimbabwe alikuwa mpiganaji wa ukombozi aliyeiongoza nchi yake kupata uhuru mwaka 1980.Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya naye ametuma risala ya pole kwa familia na Wazimbabwe ambao Mugabe aliwahudumia kwa kujitolea kwa miaka mingi. Amemtaja Mugabe kama mzalendo wa nchi yake, mpiganaji wa uhuru na miongoni mwa wakereketwa wa Afrika, mtu aliyekuwa na ujasiri na ambaye hakuogopa kupigania kile alichokiamini.

Rambirambi kama hizo pia zimetolewa na Rais John Magufuli wa Tanzania ambaye amesema bara la Afrika limempoteza mtu jasiri na kiongozi mkereketwa wa Afrika, aliyeongoza kwa kutoa mfano kwa kupinga ukoloni.

Kiongozi wa chama cha upinzani Zimbabwe, Nelson Chamisa, pia ametuma salamu za pole. Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Chamisa ameandika kuwa ni wakati wa majonzi kwa familia ya Marehemu Mugabe na kwa Zimbabwe kwani wamepoteza mtu muhimu.

Raia wengi wa Zimbabwe pia wameelezea huzuni yao kufuatia kifo cha Mugabe.

Vyanzo: Reuters, AFPE