1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Virusi vya Zika vyawa tishio kuliko ilivyodhaniwa

Lilian Mtono/ AFPE12 Aprili 2016

Waatalamu wa afya nchini Marekani wameonya kuwa virusi vya Zika vinaweza kuwa tishio kuliko ilivyofikiriwa awali, virusi hivyo vinahusishwa na dosari za kimaumbile wanazozaliwa nazo watoto.

https://p.dw.com/p/1ITwF
Brasilien Zika CDC
Picha: picture alliance/AP Photo/A. Penner

Serikali ya Marekani imewaomba watunga sera nchini humo kiasi cha Dola Bilioni 1.9 kuunga mkono juhudi za kukabiliana na virusi vya Zika, ambavyo bado vina mkanganyiko na kuhusishwa na madhara makubwa kwenye ubongo wa watoto, lakini hata hivyo ombi hilo bado halijapatiwa majibu, kutoka katika bunge linalotawaliwa na chama cha Republican.

Rais Obama ameomba kiasi hicho cha fedha kama hatua ya dharura ya kukabiliana na kuenea zaidi kwa janga la Zika kimataifa, na kujiandaa iwapo kutakuwa na kuenea zaidi nchini Marekani. Wiki iliyopita, taarifa kutoka serikalini zilisema, kiasi cha Dola Milioni 589 zilizosalia katika mpango wa kukabiliana na mripuko wa Ebola, zilipelekwa katika mapambano dhidi ya Zika.

Kupitia mbu aina ya Aedes aegypti, Zika imeendelea kuenea kwa kasi kwenye maeneo zaidi ya 30 katika ukanda wa nchi za Amerika ya Kusini na Visiwa vya Carribean tangu mwaka jana. Matukio machache yamegundulika yakionyesha virusi hivyo kuenezwa pia kwa njia ya ngono.

Upo umuhimu wa kuwa tayari, kila kitu kinachochunguzwa kuhusu mbu hawa kinatisha kuliko ilivyodhaniwa awali. Alisema Mkurugenzi mkuu msaidizi wa Kituo cha utafiti wa magonjwa, CDC Anne Schuchat kwa waandishi wa habari. Tunaendelea kujifunza kuhusu virusi hivyo kila siku, ingawa bado hatuna uhakika iwapo tunachojifunza ndicho kina uhakika, aliongeza Schuchat.

Utafiti juu ya Zika unaendelea
Utafiti juu ya Zika unaendeleaPicha: Reuters/I. Alvarado

Mkurugenzi wa taasisi ya taifa ya magonjwa ya mzio na kuambukiza Anthony Fauci, amesema bado kuna mengi ambayo bado hayajaweza kutambulika. "Kwa ujumla bado kuna mengi ya kujifunza, na tunahitaji kujifunza sana kwa sababu virusi hivi si vya kawaida kabisa" alisema.

Wataalamu bado wanajadili kitisho hicho

Mtaalamu huyo amesema, iwapo fedha hizo zilizoombwa na Rais hazitapatikana, hakutakuwepo na uwezekano wa kufikia mahali walipotaka kufikia ili kutimizia matarajio yao. "Wakati rais alipoomba Dola Bilioni 9.1, ni kweli tunahitaji kisi hicho cha fedha", alisema. Mamia kwa maelfu ya raia wa himaya ya Marekani, ya Puerto Rico wanaweza kuwa wameathirika ifikapo mwishoni mwa mwaka, afisa wa afya nchini Marekani ameonya.

Ripoti za kitafiti kutoka nchini Brazil zinaonyesha kuwa mwaka jana maambukizi kwa wanawake wajawazito yalihusishwa moja kwa moja na watoto wanaozaliwa wakiwa na vichwa vidogo na visivyo vya kawaida, pamoja na dosari nyingine ya uzazi, kitaalamu, Microcephaly, inayosababisha madhara kwenye ubongo.

CDC imeendelea kuonya wanawake wajawazito au wanaotarajia kupata ujauzito kutotembelea maeneo yaliyokwishaathirika na virusi vya Zika, kwa sababu virusi hivyo mara nyingine huenezwa kwa njia ya ngono. Aidha kituo hicho kimesema, wanaume waoliwahi kuwepo maeneo hayo wanatakiwa ama kutumia kinga ya mipira ya kiume wanapokutana na wake zao wajawazito au kutokutana nao kabisa kimwili hadi mtoto atakapozaliwa.

Zaidi ya matukio 300 ya kusambaa kwa Zika nchini Marekani yanahusishwa na watu wanaotembelea maeneo yaliyoathirika na Virusi hivyo. Wakati CDC ikitaraji kuongezeka kwa matukio mapya ya Zika, hivi sasa inashirikiana na serikali kuu na serikali za mitaa kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mbu hao.