1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Visiwa ni muhimu kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Josephat Nyiro Charo12 Juni 2014

Huku zikikabiliwa na kitisho cha kuangamia kutokana na ongezeko la kima cha bahari, nchi nyingi za visiwa vidogo vidogo zinageukia kwa kasi matumizi ya nishati inayoweza kutumika tena na tena.

https://p.dw.com/p/1CHP3
Pk Exekutivdirektor des UN - Umweltprogramms
Picha: picture-alliance/dpa

Ingawa visiwa hivi havichangii sana utoaji wa gesi ya kaboni, nchi ndogo za visiwa kama vile Barbados ziko mbele katika kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi na zinaweza kuwa nguzo muhimu kwa mataifa mengine ya dunia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

"Mataifa ya visiwa vidogo yanapaswa kusikilizwa na nchi nyingine za dunia," amesema Achim Steiner, Mkurugenzi Mgtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP. "Mataifa mengi yatakabiliwa na mabadiliko ya kimsingi. Baadhi yatapoteza asilimia kati ya 60 na 70 ya pwani zao na miundombinu mingi ya utalii. Mabadiliko ya tabia nchi yataziharibu baadhi ya nchi na kipato cha mamilioni ya watu," Steiner ameliambia shirika la habari la IPS mjini Bridgetown, Barbados.

"Siku za Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira ya dunia, lakini pia mada nyingine, kwanza kabisa ni mualiko kwa kila mtu kuangalia eneo lake analoishi, familia yake, biashara, shule, ofisi zao - je tunaweza kufanya nini? Kwa sababu hivyo ndivyo mageuzi yanavyoweza kufanyika. Mageuzi huanza na mtu mmoja."

Matumbawe yako hatarini

Hadi asilimia 100 ya matumbawe katika baadhi ya maeneo ya bahari ya Karibik yameathiriwa kutokana na maji kuwa moto mno kunakohusishwa na ongezeko la joto duniani. Pasipo mkakati wa dunia kupunguza utoaji wa gesi za viandani huenda kukakosekana matumbawe katika eneo zima la Karibik kufikia mwaka 2050, kwa mujibu wa ripoti ya shirika la UNEP kuhusu mataifa ya visiwa yanayoendelea.

Ripoti hiyo iliyotolewa Bridgetown, mji mkuu wa Barbados, wiki iliyopita, inasema mataifa ya visiwa katika eneo la Karibik yanakabiliwa na uharibifu wa pwani zake wa gharama ya dola bilioni 187 kutokana na kima cha bahari kabla mwisho wa karne hii.

Ian Somerhalder, Mchezaji filamu wa Marekani na balozi wa nia njema wa Umoja wa Mataifa.- amesema, "Natarajia kuitumia fursa hii kama balozi wa nia njema kusisitiza uhusiano muhimu uliopo na matumbawe, uhisiano kati ya matumbawe na masuala mengi mazito ya kimataifa tunayoyakabili. Kutoka kutumia raslimali kwa uangalifu zaidi hadi kupunguza matumizi mabaya na utupaji wa chakula, kuwalinda wanyama pori wetu na kuwaelimisha vijana."

Bildergalerie Dracula The Vampire Diaries
Ian Somerhalder, kulia, akiwa na wachezaji filamu wenzake, Paul Wesley na Nina DobrevPicha: picture-alliance/dpa

Ongezeko la kima cha bahari kwa sentimita 50 litakuwa na maana nchi ya Grenada itapoteza asilimia 60 ya fukwe zake. Viwango vya maji baharini vinatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa kuliko hicho, inasema ripoti ya hivi karibuni ya sayansi kuhusu kuyeyuka kwa theluji katika eneo la Antarctica na Greenland pamoja na mamia ya mito ya barafu.

Visiwa vinakabiliwa na hatari ya athari za ongezeko la joto duniani zitakazoziathiri kwa kiwango kikubwa sekta kadha wa kadha zikiwemo utalii, kilimo, uvuvi, nishati, maji safi, afya na miundombinu, ripoti hiyo imesema.

"Wakati sayari yetu inapozungumza lazima tusikilize," amesema waziri mkuu wa Barbados, Freundel Stuart. "Ulimwengu unajua jinsi ya kulipiza kisasi," Stuart ameliambia shirika la habari la IPS.

Paza sauti dhidi ya ongezeko la kima cha bahari

Kwa Barbados, Siku ya kimataifa ya Mazingira ya mwaka huu na kauli mbiu "Ongeza sauti yako na sio kima cha maji baharini" haikuwa hatua ya kusherehekea tu bali pia kujitolea kwa dhati kuwa nchi yenye uchumi unaojali mazingira zaidi Amerika Kusini na eneo la Karibik. Nchi hii yenye wakazi 275,000 inapatikana mashariki mwa eneo la Karibik, kilometa 800 kutoka pwani ya Venezuela. Ikiwa imekabiliwa na ukame wa mara kwa mara katika miongo miwili iliyopita, Barbados imelazimika kutumia mfumo wa kusafisha maji ya chumvi kwa ajili ya kunywa unaotumia kiwango kikubwa cha nishati.

Barbados tayari imekamilisha utafiti wa miaka mitatu kuhusu uchumi unaojali mazingira kutathmini kinachohitaji kufanywa. Utafiti huo umebaini kuwa sera zinazoyajali mazingira hazitoshi na kwamba Barbados pia inahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya umma na binafsi, pamoja na elimu na mabadiliko katika tabia ya watumiaji bidhaa.

"Barbados ni mojawapo ya mataifa yanayoongoza duniani katika chumi zinazojali mazingira. Visiwa vidogo vinaweza kuwa kama nguzo kwa mataifa mengine ya dunia," amesema Steiner wakati wa mahojiano na shirika la habari la IPS.

Visiwa vidogo vinahitaji msaada ikiwa ni pamoja na udhamini wa kifedha na uhamishaji wa teknolojia kutoka kwa mataifa yaliyoendelea ili kuwezesha mageuzi haya na kukabiliana na athari za sasa za mabadiliko ya hali ya hewa. Visiwa hivi vinaweza na vinataka kusonga mbele haraka kuzifanyia mageuzi chumi zao, kufunguwa nafasi za ajira zinazoyajali mazingira, kuongeza matumizi bora ya raslimali na kutumia nishati ambayo pia inayajali mazingira.

Mwandishi: Josephat Charo/IPS

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman