1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita dhidi ya ugaidi vyapata sura mpya

25 Julai 2011

Umwagaji mkubwa wa damu uliotokea nchini Norway mwishoni mwa wiki iliyopita na janga la njaa katika Pembe ya Afrika ni mada kuu mbili zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani Jumatatu ya leo.

https://p.dw.com/p/RbxL

Basi tunaanza na gazeti la MITTELBAYERISHE ZEITUNG linalosema:

Wahanga wa kitendo hicho cha ugaidi nchini Norway walikuwa na ndoto ya kuishi pamoja kwa amani. Vijana hao waliamini kuwa rangi tofauti ya ngozi au dini tofauti sio pingamizi bali ni faida kwa jamii. Kila taifa huru, lapaswa kujivunia kuwa na vijana kama hao. Ukweli kwamba watu kama hao, ndio walioteketezwa kwa sababu za chuki, ni jambo linalovunja moyo kabisa. Kitendo hicho kisicho na maana, kitupe nguvu ya kukabiliana na ugaidi. Njia, ni kupigania uhuru, uvumilivu na uwazi. Kufanya vingine ni kuwapa ushindi wafuasi wa itikadi kali.

Gazeti la HEILBRONNER STIMME likiandika kuhusu mada hiyo hiyo linaeleza hivi:

Watu wote wa Ulaya wanapaswa kutafakari kufuatia kile kilichotokea huko Norway. Na hasa, Wajerumani. Kwani, jamii yenye mchanganyiko wa tamaduni mbali mbali, ndio mustakabali wa nchi hii. Anaeamini vingine, anakwenda kinyume kabisa na wale walio na ujuzi bora zaidi. Kupuuza matamshi ya chuki na ubaguzi dhidi ya wageni, ni kuwapa uwanja wale waliopotelewa na akili.

Gazeti la SCHLESWIG-HOLSTEIN AM SONNTAG linasema kuwa kufuatia mashambulizo ya Septemba 11 2001, rais wa wakati huo wa Marekani alitoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa, kupiga vita ugaidi katika kila pembe ya dunia.

Lakini sasa vita hivyo vinaingiza sura yake ya pili - yaani vita dhidi ya itikadi kali, dhidi ya sera kali za mrengo wa kulia na wa kushoto, dhidi ya chuki ya wageni na ukosefu wa uvumilivu katika jamii. Kuna haja ya kuwa macho zaidi ili kuweza kukabiliana na maadui wa ustaarabu.

Sasa tunageukia mada nyingine inayoendelea kugonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani. Janga la njaa katika Pembe ya Afrika. Gazeti la DER TAGESSPIEGEL linauliza, kwanini ulimwengu hukawia kuchukua hatua mizozo inapoibuka kama vile hivi sasa katika Afrika Mashariki?

Kwa maoni ya gazeti hilo, sababu ni kuwa daima, habari za kitisho cha njaa zinapoibuka kwanza hutathminiwa iwapo kitisho hicho kitatoweka. Halafu michango ya fedha hutolewa kusaidia kuimarisha kilimo. Lakini msaada huo ni mdogo sana kulinganishwa na ule unaohitajiwa kwa msaada wa dharura, mtoto wa kwanza anapofariki kwa njaa. Ionekanavyo, serikali hufanya kazi kama binadamu wote. Huchukua hatua pale mzozo unapokuwa mkubwa kupindukia kiasi.

BERLINER ZEITUNG linasema hata ikiwa hatua zimekawia kuchukuliwa, leo mashirika ya misaada ya kimataifa yanayokutana mjini Rom nchini Italia, yanatazamia kupata michango ya fedha za kuwasaidia wahanga wa janga la njaa katika Pembe ya Afrika.

Mwandishi:Martin,Prema/dpea

Mhariri: Yusuf Saumu