1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita Gaza. Hamas yavurumisha makombora 3

Eric Kalume Ponda28 Januari 2009

Hali ya utulivu katika eneo la Ukanda wa Gaza bado inalegalega baada ya Hamas kuvurumisha makombora matatu alasiri ya leo dhidi ya maeneo yanayokaliwa na wanajeshi wa Isael.

https://p.dw.com/p/Gi53
Mjumbe maalum wa Rais Barack Obama George Mitchel na Rais wa Israel Shimon Pers.Picha: AP

Hatua hiyo imetekelezwa katika kile wanachokikitaja kujibu shambulio la mapema la Israel lililosababisha kifo cha Mpalestina mmoja.


Hayo yanatokeo huku mjumbe maalum wa rais Barack Obama George Mitchell, anapozuru eneo la hilo la mashariki ya kati kuendeleza juhudi kupatanisha pande hizo mbili.

Wakaazi wa eneo hilo wana hofu kwamba chokochoko hiyo huenda ikasababisha mashambulio makali kama yale yaliyofanywa na Israel mapema ndani ya Gaza kwa muda wa wiki tatu na kuwaua Wapalestina 1,300 na wengine 5000 kujeruhiwa.


Makombora hayo yaliyovurumisha na Hamas yalishambulia eneo la Mashariki mwa mji wa Maghazi ndani ya utawala huo wa Wapalestina ambako yadaiwa wanajeshi wa Israel bado walikuwa wakifanya mashambulio makali.


Mapema leo wanajeshi wa Israel walishambulia eneo moja katika mji wa mpakan wa Rafah baina ya Israel na Gaza kujibu shambulio jingine la Hamas hapo jana lililosababisha kifo cha mwanajeshi wao mmoja.


Wakati wa shambulio hilo, ndege za kijeshi za Israel zilishambulia matobwe yaani njia za chini ya ardhini zinazodaiwa kutumiwa na Hamas kuingiza silaha kimagendo ndani ya Gaza.


Matukio ya hivi punde yamesababisha waziri wa ulinzi nchini Israel kuahirisha safari yake nchini Marekani ambako alitarajiwa kukutana na mwenzake Roberts Gates.

Kadhalika, matukio hayo ya hivi punde yanatokea wakati ambapo mjumbe maalum wa Marekani, George Mitchell, amewasili nchini Israel baada ya kufanya mashauriano na Rais Hosni Mubarak wa Misri kujaribu kuokoa mpango wa amani wa mashariki ya kati.


Mitchell alifanya mazungumzo na Rais Shimon Peres katika makao yake mjini Jerusalem ambako amesisitza haja ya kuelekeza juhudi za kupatikana amani ya kudumu katika eneo hilo.


Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, ambaye alikutana na baraza la usalama nchini humo amepongeza juhudi za Marekani katika kuutanzua mzozo huo, lakini akasisitiza kuwa Israel ina haki ya kujibu mashambulizi yoyote kutoka kwa Hamas.


Wakati huo huo, Ufaransa imewasilisha malalamiko yake kwa balozi wa Israel kuhusiana na kisa ambapo wanajeshi wa Israel walifyatua angani na kuwazuia wajumbe wa Umoja wa Ulaya kwenye kituo cha mpakani cha Erez katika eneo la Gaza.


Wajumbe hao walikuwa wakirejea Jerusalem kutoka Gaza baada ya kukadiria hali ya binadamu ilivyo katika eneo hilo walipozuiliwa na wanajeshi wa Israel kwa muda wa masaa 6, kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Ufaransa, Eric Chevallier.


Umoja wa mataifa unasema kuwa zaidi ya wakaazi 900,000 katika eneo la Ukanda wa Gaza, lenye idadi ya watu milioni 1.5, sasa wanategemea misaada ya binadamu kufuatia uharibifu uliosababishwa na mashambulio ya Israel.

Ponda/Afp-Reuters