1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita kamili dhidi ya wapiganaji wenye siasa kali

Saumu Mwasimba18 Julai 2007

Rais Pervez Musharaf wa Pakistan ametangaza vita kamili dhidi ya wapiganaji ambao wameanzisha mashambulio ya kujitoa muhanga katika taifa hilo.

https://p.dw.com/p/CB2j
Rais Pervez Musharraf
Rais Pervez MusharrafPicha: AP

Tangazo la Musharraf limekuja baada ya watu 34 kuuwawa kwenye mapambano ya kufyatuliana risasi katika eneo tete la mpakani na Afghanstan ikiwa ni siku moja baada ya shambulio la kujitoa muhanga kufanywa dhidi ya mkutano wa kuipinga serikali mjini Islamabad ambapo watu wengine 17 waliuwawa.Wanajeshi 16 wameuwawa leo hii kaskazini magharibi mwa Pakistan na watu 21 kujeruhiwa katika mashambulio yaliyolenga msafara wa wanajeshi.

Rais Musharaf amesema sasa serikali yake inatangaza vita kamili dhidi vikundi vya watu wenye siasa kali nchini humo.

Amewataka wapakistan kushirikiana ili kuzuia machafuko zaidi nchini humo.Tukimnukulu alisema

‘’Tuwatenge mataliban kwa kushirikiana pamoja na watu wetu la sivyo janga kubwa linaweza kutokea kama inavyotokea Afghanstan najaribu kuzuia hali hiyo kuwatokea watu wapakistan nah ii inawezekana tu ikiwa tutawatenga wataliban’’.

Rais huyo wa Pakistan ambaye yuko katika shinikizo kubwa la Marekani la kumtaka apambane na waislamu wenye itikadi kali nchini mwake ameapa kuwashambulia wale wote wanaosababisha kuongezeka ghasia tangu wanajeshi wa serikali walipouvamia msikiti mwekundu mjini Islamabad wiki iliyopita.

Aidha Musharaf ambaye alijinyakulia madaraka mwaka 1999 kwa kufanya mapinduzi amesema hawezi kutangaza hali ya hatari licha ya umwagikaji mkubwa wa damu na kwamba ghasia hizo haziwezi kuzuia uchaguzi usifanyike mapema mwaka ujao.

Marekani imeongeza mbinyo kwa rais Musharaf ambaye ni mshirika wake mkubwa katika vita dhidi ya Ugaidi kumtaka aanzishe opresheni kamili ya kijeshi katika eneo la mkapani na Afghanstan ambako inadai wapiganaji wanajificha na wanapanga shambulio jingine kama la Septemba 11 nchini Marekani.

Hapo jana ripoti ya shirika la kijasusi la Marekani ilionya kwamba kundi la Mtandao wa kigaidi la alqaeda limejiimarisha upya nchini Pakistan na limepania kufanya mashambulio yatakayoleta maafa makubwa kabisa nchini Marekani.

Pakistan imesema kufikia mwishoni mwa mwaka ujao itatuma Polisi pamoja na wanajeshi 30 elfu katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo kupamabana na wapiganaji wenye itikadi kali.

Wakati ikiaminika kuwa wapiganaji wanalipiza kisasi dhidi ya Musharaf na serikali yake kwa kuuvamia msikiti wa Lal Masjid na kumuua kiongozi wake pamoja na wafuasi, wapiganaji wengine wanaunga mkono kundi la Taliban kaskazini mwa jimbo la Wazirstan wameapa kuvishambulia vikosi vya usalama baada ya kukataa mpango wa amani.