1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya biashara kati ya Marekani na China Magazetini

Oumilkheir Hamidou
7 Agosti 2019

:Mgogoro wa biashara kati ya China na Marekani na madhara yake kwa dunia na mjadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/3NUX3
China Wechselkurs Yuan US-Dollar
Picha: AFP

Tunaanza na mgogoro unaotishia kugeuka vita vya kibiashara kati ya Marekani na China. Gazeti la "Augsburger Allgemeine" linazungumzia ukakamavu wa rais wa Marekani na kuandika:" Trump anacheza mchezo wa hatari ambao madhara yake hakuna anaeweza kuyakadiria. Mbaya zaidi ni kwamba hajali yote hayo. Chuki zote alizo nazo, hakuna neno jengine tukizingatia risala zake kupitia mtandao wa twitter, anazitoa dhidi ya china. Anaongoza vita vya biashara dhidi ya nchi hiyo tena kwa namna ambayo mpaka wawekezaji wa kimarekani wanapata shida. Kwasababu vita vya kibiashara vinavyochochewa na  hatua za kila mara za kuzidisha makali ya ushuru wa forodha zinatishia pia kusababisha vita vya sarafu."

Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linamulika uamuzi wa China wa kushusha thamani ya sarafu yake. Gazeti hilo linaandika. "Viongozi wa mjini Peking wanapopunguza thamani ya sarafu yao kulingana na Dollar, cha mwanzo kubadilika ni bei za biashara kati ya Marekani na China. Lakini nchi nyengine za Asia zinaweza pia kupunguza thamani ya sarafu zao dhidi ya Dola ili kuleta uwiano katika mashindano ya kibiashara pamoja na China. Kitakachofuatia mchezo huo tayari kinajulikana-kama ilivyoshuhudiwa katika mchezo wa kupandisha ushuru kila mara-kwa maneno mengine hakuna atakaefaidika-kinyume kabisa, kila mmoja atalazimika kumeza machungu ya kuporomoka ukuaji wa kiuchumi ."

Juhuddi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Nchini Ujerumani mjadala umepamba moto watu wakijiuliza nini cha kufanya ili kukabailiana na mabadiliko ya tabianchi. Gazeti la "Oberhessissche Presse" linazungumzia mjadala huo na kuandika: "Walinzi wa mazingira wanakuwa wanachukiwa na watu wanapohimiza kwa mfano idadi ya mifugo ipunguzwe, pawepo hatua maalum kuhusu mwendo wa kasi wa magari au kodi izidishwe kwa magari yanayotumia mafuta mengi. Lakini kwa kufanya hivyo wanachochea mjadala muhimu: Jamii iko tayari kuachana na kitu gani ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi? Na wapi hawako tayari? Suala muruwa lakini wengine wangesema halitilii maanani masilahi ya jamii. Hatua za kupandisha bei ya nishati kwa mfano zitawaathiri zaidi wale wanaoishi katika nyumba za kizamani na hawamudu kununua magari. Hata hivyo mjadala ni muhimu ili kuweza kuona jinsi jamii inavyoweza kuchangia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga