1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya chacha Jamuhuri ya Afrika ya Kati

28 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBne

Hali ni tete katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati kufuatia kuzuka kwa ghasia na ongezeko la visa vya kihalifu. Maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makwao na kutafuta hifadhi kwingineko hasa kaskazini mwa taifa hilo ambako vita vimechacha.

Vita hivyo kati ya majeshi ya serikali na waasi vimewaacha wenyeji wengi katika hali ya kutatanisha. Wengi wao wamelazimika kukimbilia nchi jirani ya Chad katika muda wa wiki kadhaa zilizopita huku ikisiwa elfu 50 yao wamejificha msituni. Inadaiwa kuwa majeshi ya serikali yamekuwa yakiwaua wanaume na vijana wanaowashuku kuunga mkono makundi ya waasi na hata kuteketeza nyumba zao. Na umri si hoja kwani majeshi hayo yamekuwa yakiwaua vijana hata wa kati ya umri wa miaka miwili na mitatu.

Godfrey Byaruhanga ambaye ni mtafiti wa shirika la kutetea haki za kibinadamu Amnesty International alikuwa huko hivi majuzi na anasema haya...

"Serikali kwa upande wake imeshindwa kwani majeshi yake yanatumika katika kugandamiza haki za wenyeji wa taifa hilo. Majeshi hayo yamekuwa yakiwaua watu ovyoovyo".

Raia wa Taifa hilo wameamua hata kutorokea nchi kama Sudan, kusini mwa Chad na Cameroon ambako pia wamekuwa wakikabiliwa na matizo si haba. Rais wa taifa hilo lililo miongoni mwa yale maskini zaidi ulimwenguni Francois Bozize mara kwa mara amekuwa akiyashtumu makundi hayo ya waasi kwa vurugu ambazo zimekuwa zikiendelea.

Lakini hali katika jamuhuri ya afrika ya kati kwa kiasi kikubwa imefunikwa na hali iliyovyo katika eneo la, Darfur, ambako serikali ya sudan imeshtumiwa na marekani kutekeleza mauji ya halaiki dhidi ya wasudan weusi mauji yanayotekelezwa na wa sudan wenye asili ya kiarabu.

Ufaransa ambayo imekuwa ikingilia kati mapigano hayo tangu Jamuhuri ya afrika ya kati kupata uhuru mwaka wa 1960 ina karibu wanajeshi 200 katika mji wa Bangui. Marekani ambayo ilimwondoa balozi wake nchini humo mwaka 2002 kutokana na kutoridhishwa na maongozi ya aliyekuwa rais wa taifa hilo Ange-Elix Patasse kisaisa na kiuchumi itamrejesha tena balozi wake mpya Fredrick Cook mwezi ujao.

Patasse ambaye alichaguliwa rais mwaka 1993 nafasi yake alichukliwa na Bozize kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 2003. Hata hivyo mwezi Mei mwaka wa 2003 uchaguzi mkuu ulifanyika na Bozize kuibuka mshindi.Kwa mujibu wa Cook uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.

Kundi moja la waasi ,the popular Army for the Restoration of Democracy linaaminika kumuunga mkono Patasse.Hata hiyo kiongozi wake aliwafichulia wanahabari mapema wiki hii kuwa yenye pamoja na wenzake kadhaa wanajitayarisha kuweka chini silaha zao na kujiunga na jeshi la serikali.

Kulingana na shirika la kutetea haki za kibinadamu Amnesty International hali imezorata zaidi katika miezi kadhaa iliyopita. Mapema mwezi huu mfanyikazi mmoja raia wa ufaransa kutoka kundi la madaktari wasiokuwa na mipaka aliuawa alipokuwa katika shughuli za kikazi nchini humo. Mauji hayo yalipelekea baadhi ya mashirika la kutoa misaada kusitisha shughuli zao katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na vita hivyo.